November 24, 2024

Unayotakiwa kufahamu kuhusu tuzo za dijitali zilizozinduliwa Tanzania

Lengo kubwa la kuanzisha tuzo hizo ni kutambua, kutunza ubunifu, uvumbuzi na ufanisi katika utumiaji wa teknolojia Tanzania.

  • Lengo kubwa la kuanzisha tuzo hizo ni kutambua, kutunza ubunifu, uvumbuzi na ufanisi katika utumiaji wa teknolojia Tanzania.
  • Zimeanzishwa kwa mara ya kwanza na kampuni ya Tanzania
  • Zimegawanyika katika makundi kuu 9 na vipengele 50 ikiwemo Serikali mtandaoni na maendeleo na diplomasia mtandaoni.

Dar es Salaam. Kwa mara ya kwanza, kampuni ya Serengeti Bytes ya Tanzania imeanzisha tuzo za digitali zinazohusisha watu binafsi, mashirika na taasisi zinazotumia teknolojia ya kidigitali ili kuchagiza uwajibikaji na ubunifu katika shughuli za maendeleo. 

Mkuu wa Programu, Utafiti na Uvumbuzi wa kampuni hiyo ya mawasiliano na mahusiano ya umma, Genos Martin aliyekuwa akizungumza jana (Januari 16, 2020)  katika uzinduzi wa tuzo hizo jijini Dar es Salaam, amesema lengo kubwa la kuanzisha tuzo hizo ni kutambua, kutunza ubunifu, uvumbuzi na ufanisi katika utumiaji wa teknolojia Tanzania.

“Tuzo hizi ni za kipekee kwa kutambua na kutunza juhudi za kidigitali nchini. Tunatazamia kuunga mkono na kuchochea juhudi zinazofanyika kuleta matokeo chanya katika mitandao,” amesema Genos.

Tuzo hizo ambazo zinachagiza uwajibikaji, ubunifu na uvumbuzi kidijitali zimegawanyika katika makundi makuu tisa ya Serikali mtandaoni, maendeleo na diplomasia mtandaoni, masoko mtandaoni, burudani mtandaoni, vyombo vya habari mtandaoni, uvumbuzi wa kidigitali, mawasiliano ya kidigitali, uchambuzi mtandaoni na tuzo ya jumla la chaguo la watu.

Sambamba na makundi makuu, kuna vipengele 50 vilivyopo katika tuzo ambavyo vitashindaniwa vikiwemo, runinga bora ya kidigitali, blogubora ya habari na radio bora ya mtandao.

Hiyo inaweza kuwa fursa muhimu kwa vyombo vya habari vya mtandaoni kutambuliwa katika kazi wanazofanya za kuelimisha, kuburudisha na kuhabarisha umma wa Watanzania.  


Zinazohusiana:


Tuzo hizo ziko wazi kwa kampuni, mashirika, watu binafsi na taasisi za kijamii, mashirika ya maendeleo na taasisi zinazofanya kazi Tanzania. 

Mchakato wa kuteua washindani kwa kila kipengele utafanyika mtandaoni kwa kupigiwa kura na watu na uamuzi wa majaji watakaosimamia shughuli hiyo.

Hata hivyo, mchakato wa mapendekezo na kupiga kura umeshaanza kufanyika toka Januari 15 ,2020 kupitia tovuti yao ya www.digitaawards.c.tz na utamalizika ifikapo Februari 15 ,2020. 

Washindi watatangazwa Machi 10, 2020 na watapewa vyeti vya kuwatambua na zawadi zingine kama zitakavyoamuliwa.