July 5, 2024

Unyanyasaji wachangia kuwakimbiza wasichana kwenye mitandao ya kijamii

Msichana mmoja kati ya watano duniani amepunguza au ameacha kutumia kabisa mitandao ya kijamii kutokana na unyanyasaji unafanyika mtandaoni.

  • Msichana mmoja kati ya watano duniani amepunguza au ameacha kutumia kabisa mitandao ya kijamii kutokana na unyanyasaji unafanyika mtandaoni. 
  • Unyanyasaji huo unaotokea zaidi Facebook unawanyima fursa wasichana kupata fursa za mtandaoni na uongozi.
  • Kampuni za mitandao ya kijamii zatakiwa kuchukua hatua kudhibiti unyanyasaji huo. 

Dar es Salaam. Utafiti mpya wa Shirika la kimataifa linaloshughulikia masuala ya watoto na wasichana, Plan International umebaini kuwa msichana mmoja kati ya watano duniani amepunguza au ameacha kutumia kabisa mitandao ya kijamii kutokana na unyanyasaji unafanyika mtandaoni. 

Hali hiyo inachangia kuwafanya wasichana kutokuwa na nguvu katika ulimwengu unaokuwa kidijitali na kuathiri uwezo wao wa kuonekana, kusikilizwa na kuwa viongozi katika ngazi za maamuzi.

Utafiti huo wa uhuru wa kuwa mtandaoni (Free to be online? Girls’ and young women’s experiences of online harassment) uliochapishwa Oktoba 4, 2020  uliwashirikisha wasichana na wanawake 14,000 wenye umri kati ya miaka 15 hadi 25 kwenye nchi 22, ikiwemo Brazil, Benin, Marekani, Nigeria, Uhispania, Thailand na India. 

Ripoti ya utafiti huo inaeleza kuwa zaidi ya nusu (asilimia 58) ya wasichana  wamekumbana na unyanyasaji wa mitandaoni.

Unyanyasaji hutokea zaidi wanapotumia mtandao wa Facebook, ambapo asilimia 39 ya wasichana waliohojiwa wanasema walipata manyanyaso kupitia mtandao huo wenye watumiaji zaidi ya bilioni 2.6 duniani. 

Kutokana na unyanyasaji huo ambao ni sehemu ya ukatili wa kijinsia, wasichana hutumia njia ya kupunguza au kaacha kabisa kutumia mitandao ya kijamii ili kuepuka vitendo hivyo ambavyo huathiri maisha yao ikiwemo afya ya akili. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, asilimia 19 au sawa na kusema msichana mmoja kati ya watano amepunguza au ameacha kabisa kutumia mitandao ya kijamii huku asilimia 12 wakibadilisha namna ya kuwasilisha mawazo yao wanapokuwa mtandaoni. 

Unyanyasaji waliokumbana nao wasichana hao ni pamoja na kudhalilishwa kwa makusudi ambapo asilimia 41 waliathirika, asilimia 39 ya wasichana walikumbana na lugha za matusi, kuchekwa maumbile yao pamoja na vitisho vya unyanyasaji wa kijinsia. 

Utafiti huo umebaini kuwa hapakuwa na maeneo sahihi ya kuripoti kuhusu kuzuia unyanyasaji wa mtandaoni ambao unahusisha ujumbe wa chuki, picha za ngono pamoja na kuwafuatilia watu kwa siri.

Hata hivyo, utafiti huo unaeleza kuwa mitandao ya kijamii ni sehemu muhimu kwa wasichana kujifunza mambo mapya na kukutana na marafiki ili kubadilishana mawazo, lakini wanapokutana na unyanyasaji wanakosa fursa ya kuzifikia ndoto zao. 


Soma zaidi:


Hatua zichukuliwe kuwaokoa wasichana mtandaoni

Nchini Tanzania, kampeni mbalimbali za kuwalinda wasichana na wanawake dhidi ya ukatili wa kijinsia zimeanzishwa ikiwemo za @WomenAtWebTZ na @jeshiladada. 

Kampeni hizo zimekuwa zikitoa mafunzo kwa kundi hilo kufahamu kwa undani matumizi ya mitandao ya kijamii na namna ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia wakati huo huo wakitumia mitandao hiyo kujinufaisha kwa fursa mbalimbali za elimu. 

Mtendaji Mkuu wa Plan International, Anne-Birgitte Albrectsen amezitaka kampuni za mitandao ya kijamii kuchukua hatua kulishughulikia tatizo hilo huku Serikali za nchi mbalimbali zikitakiwa kutunga sheria na kutoa matamko yatakayosaidia kupunguza  unyanyasaji wa mitandaoni. 

“Mitandao ya kijamii ina nguvu ya kufanya mabadiliko. Wanatakiwa kufanya zaidi kukabiliana na tabia hatarishi ili kuhakikisha majukwaa yao yanakuwa na mazingira salama kuwawezesha wasichana, wanawake na makundi mengine kuwa huru kujieleza,” amesema Albrectsen.