November 24, 2024

Upo tayari kununua simu ya mkononi ya zaidi ya Sh4 milioni?

Ni moja ya toleo la mfululizo wa simu za Samsung Galaxy S10 zenye uwezo wa kuhifadhi taarifa hadi TB1 na zinatarajiwa kuwa kimbilio kwa wale wanaohifadhi data nyingi kwenye simu zao.

  • Ni moja ya toleo la mfululizo wa simu za Samsung Galaxy S10 zenye uwezo wa kuhifadhi taarifa hadi TB1 na zinatarajiwa kuwa kimbilio kwa wale wanaohifadhi data nyingi kwenye simu zao.
  • Simu hizo zina uwezo wa WiFi 6 na itakuwa imeshaunganishwa tayari na mfumo wa intaneti wa 5G.
  • Suala la chaji hadi kutumia umeme sahau, ukikwama utakuwa na uwezo wa kutumia vifaa vingine kuchajia simu yako kama saa mkononi ya kidijitali.

Wapenzi wa picha nzuri katika simu ni wakati wa kuvunja kibubu baada ya kampuni ya Samsung kuzindua simu mpya za Galaxy S10 ambazo miongoni mwa sifa kubwa ni uwezo wa kuhifadhi taarifa nyingi hadi kiwango cha GB1,000 ama terabaiti moja (TB1).

Simu hizo mpya za Galaxy S10 zimezinduliwa Februari 20, 2019 ikiwa ni miaka 10 tangu kampuni ya Samsung ianze kutoa mfululizo wa simu zao.

Galaxy S10 imekuwa simu yenye uwezo mkubwa kuzalishwa na Samsung na inatarajiwa kuingia sokoni mwezi Machi mwaka huu.

Ili kuzipata simu hizo, lazima mfuko wako uchanike kidogo kutokana na gharama kubwa inayotokana ma uwezo wake mkubwa wa kuhifadhi vitu na teknolojia iliyotumika katika kuitengeneza ikiwa ni ya juu kuliko matoleo yaliyopita.

Katika nchi za Ulaya, simu za Galaxy S10e ama Lite zenye uwezo wa kuhifadhi taarifa wa 128GB kwa sasa bei yake ni wastani wa Dola 750 za Marekani sawa na Sh1.8 milioni wakati toleo lenye uwezo wa 256GB likiuzwa Dola za Marekani 850 zaidi ya Sh2 milioni.

Hata hivyo, toleo la Samsung Galaxy S10 lenye uwezo wa kuhifadhi taarifa wa 128GB itauzwa Sh2.1 milioni na milioni 2.7 kwa yenye uwezo wa  512GB. 

Kamera za Galaxy S10 zina kamera zenye lenzi tatu zitakazokusaidia kupata matukio vizuri wakati wowote katika uhalisia wake.Picha|Mtandao.

Mbali na toleo hilo, wanaotaka Samsung Galaxy S10 Plus  yenye uwezo wa  128GB basi watalazimika kuwa na Sh2.3 milioni za kitanzania kuweza kuimiliki simu hiyo. 

Lakini kubwa zaidi katika ubunifu wa simu hizo za Galaxy S10 Plus ni uwezo wa kuhifadhi taarifa nyingi zaidi katika viwango vya GB 512 na kiwango cha juu zaidi ikiwa GB1,024 ama maarufu terabaiti moja (TB1). 

Toleo hilo ndilo linauzwa ghali zaidi ikiwa ni kati ya Dola za Marekani 1,250 (Sh2.9 milioni) kwa zile zenye GB512 na Dola za Marekani 1,600 ama Sh3.8 milioni kwa zile zenye TB1. Iwapo masuala mengine ya kikodi na gharama nyingine yatahusishwa, simu hizo zitakapoingia nchini huenda zikifikia hadi gharama ya Sh4 milioni.

Kwa sasa, simu hizo huenda ndiyo ghali duniani zikizidi bei za iPhone XS Max licha ya kuwa zipo katika hatua ya awali ya wateja kuomba wauziwe (Pre-order).


Hata hivyo, bei hizo zinaendana na teknolojia ya kisasa iliyotumika kuzitengeneza simu hizo ikiwemo uwezo wa kukaa na chaji muda mrefu na kuweza kuchaji kupitia vifaa vingine pasipo kuweka kwenye umeme kama saa za kidijitali. Iwapo chaji imeisha na huna chaja jirani, unaweza kuomba kuchaji kupitia kifaa kingine kama simu janja nyingine au saa ya mkononi yenye uwezo huo.


Kwa wanaopenda picha nzuri hasa wanahabari na wazalishaji wengine wa maudhui, kwa simu hiyo mpya hawatakuwa na shida tena kwa sababu imetengenezwa kwa uwezo kama wa kamera maalum za picha.

Vilevile ina uwezo wa kuchukua picha kwa mbali bila kupoteza uhalisia wake kutokana na lensi yake ya teknolojia ya juu.

Miongoni mwa sifa nyingine kubwa ambazo wachambuzi wameziangazia zaidi ni uwezo mkubwa wa kunasa mtandao wa intaneti yenye kasi ya (WiFi 6) popote ulipo na tayari imetengenezwa kupata huduma ya 5G hata kabla teknolojia haijaanza kutumika katika mataifa mengi duniani. 

Inaelezwa kuwa hata wale ambao hawajafikiwa na huduma ya intaneti ya kasi ya 5G bado simu hizo zitakuwa na kasi kubwa katika matumizi ya mtandao.


Zinazohusiana: Apple waingiza sokoni simu mpya zinazotumia mfumo wa ‘eSIM’

                        Usiyoyajua kuhusu mtandao wa 5G



Inasadikika kuwa simu hizo zitakuwa na teknolojia ya juu ya kizazi kijacho yaani ‘Next Generation’ ikiwa ni uwezo mkubwa kuliko matoleo yaliyopita kutoka kampuni ya Samsung. 

Baadhi ya wapenzi wa simu kali wameeleza kuwa teknolojia hiyo ni ya juu na nzuri ila wanaofu kuwa watu wachache nchini wanaweza kuzimudu kutokana na gharama kubwa.

“Hii simu ina bei kubwa sana japo ina uwezo mkubwa wa kamera na nafasi…watanunua wachache kama ilivyokuwa kwa iPhone X,” amesema Hamadi Juma, mkazi wa Kinondoni, Jijini Dar es Salaam.

Kampuni ya simu za mkononi ya Tigo imetangaza leo (Februari 22, 2019) kuwa inapokea oda ya watu wanaotaka kuzinunua simu hizo.