April 4, 2025

Vodacom kumalizana na wateja wao nyumbani

Kupitia teknolojia, mteja atakuwa na uhuru wa kujihudumia mwenyewe popote alipo bila msaada wa huduma kwa wateja.

  •  Wateja watakuwa na uwezo hata wa kurudisha akaunti ya M-pesa ikiwa simu imepotea bila kwenda katika kituo cha huduma kwa wateja.
  • Mteja atakuwa na uhuru wa kujihudumia mwenyewe popote alipo bila msaada wa huduma kwa wateja.
  • Kampuni hiyo, iliyoorodheshwa kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) yajipanga kuwapa elimu wateja juu ya matumizi sahihi ya data ili kuwa na uwanja mpana wa matumizi ya simu.

Dar es Salaam. Sasa watumiaji wa mtandao wa simu za mkononi wa Vodacom Tanzania hawatapata tabu tena ya kupiga simu au kutembelea maduka ya mtandao huo ili kupata huduma kwa wateja kwa sababu teknolojia imerahisisha upatikanaji wa huduma hiyo. 

Hatua hiyo imekuja baada ya Vodacom Tanzania kuzindua kampeni ya ‘Naweza na Vodacom’ inayowawezesha wateja kupata huduma muhimu za mawasiliano kwenye simu zao wakiwa popote nchini. 

Mkurugenzi wa huduma kwa wateja, Harriet Lwakatare aliyekuwa akizungumza na Wanahabari leo (Februari 19,2019) Jijini Dar es Salaam amesema kuwa wameamua kutumia teknolojia kuwafikia wateja wake popote walipo ili kuwaondolea usumbufu wa kusaka huduma muhimu za mawasiliano.

“Ukiwa nyumbani unaweza kupata taarifa zozote bila kufuata sehemu za huduma kwa wateja au kupiga simu kuwasiliana na mtu wa huduma kwa wateja,” amesema Lwakatare.

Kutoka kulia ni Mkurugenzi wa Uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Rosalynn Mworia, Mkurugenzi Idara ya huduma kwa wateja, Harriet Lwakatare (Katikati) na Mkuu wa idara ufanisi kwa wateja, Najenjwa Mbaga wakati wakiongea na Wanahabari kuhusu kampeni mpya ya “Naweza na Vodacom” leo jijini Dar es Salaam. Picha| Zahara Tunda.

Kampeni hiyo inayolenga kuimarisha uhusiano na wateja, itawaweza watumiaji wa mtandao huo kupata huduma mbalimbali ikiwemo kurejesha namba ya siri iliyopotea au uliyosahau, kuangalia salio la vifurushi na kuwapa dondoo za taarifa za kampuni hiyo. 

Wateja wengine watakaofaidika ni wale wanaotumia huduma za fedha kwa njia ya simu ambapo kupitia mfumo wa IVR (Interactive Voice Response), watakuwa na uwezo hata wa kurudisha akaunti ya M-pesa ikiwa simu imepotea bila kwenda katika kituo cha huduma kwa wateja.

Pia mteja atakuwa na uwezo wa kusitisha muamala uliokosewa na kuondoa usumbufu wa kupoteza pesa mara kwa mara.

Katika kuhakikisha kuwa matumizi hayo ya teknolojia yanafanikiwa, Lwakatare amesema watatoa elimu na mbinu mbalimbali za kuwasaidia wateja wao kufaidika na mfumo huo mpya wa kidijitali.


Zinazohusiana: Vodacom, Mastercard zaangazia biashara ya mtandaoni kupitia Virtual Card

                         Window 95 yaja kivingine baada kutoweka sokoni kwa miaka 18


Lwakatare amebainisha kuwa wanatumia vizuri fursa ya mitandao ya kijamii katika kutoa ufafanuzi wa changamoto yoyote ya mteja kupitia  kurasa zao za Twitter, Facebook, Instagram na tovuti ambapo mtu anaweza kuuliza swali lolote linalohusu Vodacom na kujibiwa moja kwa moja.

“Kwenye tovuti yetu kuna ‘live chat’ ambayo mtu ataweza kuongea au kujibiwa na mtu kutoka Vodacom hapo kwa hapo,” amesema Lwakatare.

Hatua hiyo ya Vodacom inatajwa kama njia ya kuendeleza ushindani katika soko la mawasiliano nchini, ikizingatiwa kuwa kampuni ya Tigo tayari inatumia huduma kama hiyo hasa kuwarahisishia miamala watumiaji wa TigoPesa.