November 24, 2024

Wabuni jukwaa la kidijitali kukusanya takwimu za chakula duniani

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani (WFP) limezindua jukwaa la kidijitali la “HungerMapLIVE”, ambalo litakusanya takwimu muhimu kuhusu hali ya uhakika wa chakula katika nchi zaidi ya 90 duniani ikiwemo Tanzania.

  • Jukwaa hilo la “HungerMapLIVE” limezinduliwa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP).
  • litakusanya takwimu muhimu kuhusu hali ya uhakika wa chakula katika nchi zaidi ya 90 duniani.
  • Pia linatoa taarifa zingine muhimu kama masuala ya hali ya hewa, idadi ya watu, mizozo, lishe na hali ya majanga ya asili kama ukame.

Huenda tatizo la upatikanaji wa chakula cha uhakika katika maeneo mbalimbali duniani  likapungua, baada ya wabunifu kubuni ramani ya kidijitali inayoonyesha hali ya chakula na hatua za kuchukua kuokoa maisha ya watu.

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani (WFP) jana (Januari 22, 2020)  limezindua jukwaa la kihistoria la kidijitali la “HungerMapLIVE”, ambalo litakusanya takwimu muhimu kuhusu hali ya uhakika wa chakula katika nchi zaidi ya 90 duniani ikiwemo Tanzania.

Kwa mujibu wa WFP, takwimu za kila siku siyo tu zitasaidia kupima kwa uhakika hali ya njaa bali pia zitasaidia kufanya maamuzi ya msingi ili kuokoa maisha ya watu 

Jukwaa hilo “HungerMapLIVE” ni mfumo mpya wa kimataifa wa WFP wa kufuatilia na kutoa makadirio ya hali ya uhakika wa chakula kote duniani na kila mtu anaweza kupata fursa ya kuangalia kupitia tovuti ya hungermap.wfp.org.

Jukwaa hilo lililoanza kufanya kazi limeandaliwa kwa ushirikiano wa WFP na kampuni ya kompyuta inayoongoza China ya Alibaba ijulikanayo kama Alibaba Cloud.

Mbali ya kwamba jukwaa hilo ni chanzo cha kupata tarifa kuhusu uhakika wa chakula, pia linatoa taarifa zingine muhimu kama masuala ya hali ya hewa, idadi ya watu, mizozo, lishe na hali ya majanga ya asili kama ukame.

“Ni jukwaa la mabadiliko, na ni nyenzo ambayo inatoa elimu kuhusu moja ya changamoto kubwa zaidi zinazoikabili dunia hivi sasa, njaa ya kimataifa. Kuwa na takwimu sahihi, za wakati muafaka katika hali yoyote inayoendelea ya mgogoro kunasaidia kuongeza fursa ya mafanikio ya kupambana na njaa,” inaeleza WFP katika taarifa ya Radio ya Umoja wa Mtaifa (UN).

Kazi kubwa ya jukwaa hilo ni kuangazia watu walio na upungufu wa chakula katika nchi ambazo WFP inafanya operesheni zake na hasa katika nchi za kipato cha chini na cha wastani na kuruhusu kufahamu hali inavyobadilika siku hadi siku au mwezi hadi mwezi.

Hadi kufikia sasa WFP inasema zaidi ya watu bilioni moja ambao ni sawa na mtu 1 kati ya 7 duniani hawana chakula cha kutosha. 

“Na hii inamaanisha kwamba hawana lishe ya kutosha au wako katika hatihati ya kutokuwa na uhakika wa chakula, na mbali ya kukosa chakula cha kutosha hawana uchaguzi wa lishe bora kwa ajili ya kuwa na maisha yenye afya,” inaeleza taarifa ya UN.


Soma zaidi:


Manufaa ya jukwaa hilo

WFP imesema jukwaa hilo linaweza kusaidia kupunguza muda wa kukabiliana na majanga, kufanikisha operesheni, kupunguza gharama na kuziba pengo la taarifa katika jumuiya ya wahudumu wa misaada ya kibinadamu. 

Mbali ya kukusanya taarifa kutoka katika vyanzo mbalimbali vya umma kila siku , HungerMapLIVE inaweka mashine ya kujifunza ya akili bandia (AI) ili kutoa makadirio ya hali ya sasa ya uhakika wa chakula katika maeneo ambako takwimu ni vigumu kupatikana.