November 24, 2024

Wadau mtandaoni watoa neno WhatsApp kudhibiti habari za uongo

Wamesema hatua hiyo itakuwa na matokeo mchanganyiko ikiwemo kuathiri baadhi ya watu ambao wanatumia mtandao huo kwa nia njema.

  • Wamesema hatua hiyo itakuwa na matokeo mchanganyiko ikiwemo kuathiri baadhi ya watu ambao wanatumia mtandao huo kwa nia njema. 
  • Wengine wadai itaondoa changamoto ya mfumo wa utendaji hasa kusimamia maudhui yasiyofaa.

Dar es Salaam. Kufuatia mtandao wa WhatsApp kutangaza nia kuwapunguzia wateja wake uwezo wa kutuma ujumbe mmoja mara nyingi, wachambuzi wa masuala ya teknolojia wamesema hatua hiyo itakuwa na matokeo mchanganyiko ikiwemo kuathiri baadhi ya watu ambao wanatumia mtandao huo kwa nia njema. 

Uongozi wa mtandao huo umeeleza kuwa mabadiliko hayo yatasaidia kukabiliana na  watu wanaosambaza habari za uzushi na uongo ambazo zimekuwa zikiathiri maisha ya watu kiuchumi, kijamii na kisiasa. 

Uamuzi huo ulifikiwa siku ya jumatatu (Januari 21, 2019) baada ya majaribio ya miezi sita ya ukomo wa kutuma ujumbe yaliyofanyika nchini India ambapo unaondoa utaratibu wa zamani ambao ulikuwa unampa fursa mtumiaji kutuma ujumbe mmoja mara 20 kwa siku. 

Mtumiaji wa mtandao huo atakuwa na ukomo wa kutuma (forward) ujumbe mmoja mara tano kwa siku kwa watu binafsi na makundi ya WhatsApp.

WhatsApp inayomilikiwa na mwanzilishi wa mtandao wa kijamii wa Facebook, Mark Zukerberg imesema utaratibu huo utatumika kwa wateja wake wote wanaofikia bilioni moja katika zaidi ya nchi 180 duniani.

Mtumiaji wa mtandao huo atakuwa na ukomo wa kuutuma (forward) ujumbe mmoja mara tano kwa siku kwa watu binafsi na makundi ya WhatsApp. Picha| The Jakarta Post

Wachambuzi hao wameiambia www.nukta.co.tz kuwa uamuzi huo wa WhatsApp utakuwa na matokeo tofauti hasa kwa watumiaji kwasababu kila mtumiaji ana lengo lake la kuwasiliana kupitia mtandao huo ambao umejipatia umaarufu mkubwa hasa kwa vijana. 

Mdau wa mitandao ya kijamii, Kanney Mmari amesema kuwa mabadiliko hayo ya WhatsApp anayatazama katika pande mbili kwanza upande chanya kwa maana ya kupunguza taarifa za uzushi zinazosambazwa na watu wasio na nia njema. 

“Kutokuwa na kikomo katika kutuma jumbe katika whatsApp kulirahisisha taarifa za uongo kuenea kirahisi kuliko sasa ambapo mtu mmoja hataweza kutuma jumbe zaidi ya tano,” anasema Mmari.

Hata hivyo, anasema mabadiliko hayo yatakuwa na athari hasi hata kwa wale ambao walikuwa wanatumia mtandao huo kwa nia njema ikiwemo kupeleka habari sahihi na kutangaza biashara zao.

Changamoto itakayowapa ni kukosa uwanja mpana wa kusambaza taarifa zao kwa watu wengi kwasababu watakuwa na nafasi tano tu kwa siku.


Zinazohusiana:


Mtaalamu wa programu za kompyuta kutoka kampuni ya Code for Africa (CFA), Clemence Kyara amesema hatua hiyo imekuja wakati mwafaka kwasababu mtandao huo una changamoto ya mfumo wa utendaji ukilinganisha na mitandao mingine kama Facebook. 

Amesema tofauti na Facebook, jumbe nyingi za WhatsApp zinafanyika kwa faragha (private) jambo linalowapata changamoto wasimamizi wa mtandao huo kubaini makosa na maudhui yasiyofaa. 

“Inazuia wasimamizi kuona kinachoendelea (mazungumzo) na kuingilia kati,” amesema Kyara. 

Mabadiliko hayo yanaibua maswali mengi ikiwa yataleta matokeo yaliyokusudiwa, ikizingatiwa kuwa yamefanyika ikiwa imepita miezi sita tangu kuanzishwa kwa programu hiyo inayowawezesha watumiaji kuutuma ujumbe mmoja kwa  watu wengi na makundi mbalimbali ya mtandao huo. 

Lakini WhatsApp imesisitiza kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza utumaji wa ujumbe kwa asilimia 25 na zaidi ya nusu ya jumbe hizo zitapungua nchini India ambayo ina viwango vikubwa vya kutuma ujumbe (forwarding) duniani.