November 24, 2024

Wadau washauri Serikali kuongeza kasi ya kufundisha Tehama kwa walimu

Serikali imeshauriwa kuwaongezea uwezo wa kiteknolojia walimu wa shule za msingi na sekondari ili kuhakikisha wanafunzi wanapata maarifa na ujuzi utakaowawezesha kuwa wabunifu na kutatua changamoto zinazowazunguka.

  • Kasi hiyo hiyo itasaidia kuwaongezea maarifa ya teknolojia ambayo yanahitajika kwa wanafunzi.
  • Pia yatawawezesha wanafunzi kuwa wabunifu na kutatua changamoto za jamii zinazowazunguka.

Dar es Salaam. Serikali imeshauriwa kuwaongezea uwezo wa kiteknolojia walimu wa shule za msingi na sekondari ili kuhakikisha wanafunzi wanapata maarifa na ujuzi utakaowawezesha kuwa wabunifu na kutatua changamoto zinazowazunguka.

Akizungumza kwenye mjadala wa masuala ya elimu na teknolojia (EdTech meetup) uliofanyika Jijini Dar es Salaam, Septemba 6 2019, Mkurugenzi Mwanzilishi wa taasisi ya The Launchpad, Henry Kulaya amesema jamii inawahimiza vijana kujiajiri pasipo kuangalia kama mfumo wa elimu umewazaidia kuwa jengea ujuzi wa teknolojia kujiajiri.

Kulaya amesema changamoto iliyopo katika elimu nchini, bado walimu hawajapewa uwezo wa kutosha wa teknolojia kuwarithisha wanafunzi wanaowafundisha, jambo linalochangia wasifaidike na ujuzi wanaoupata  

Wadau wengine wamesema, walimu hasa wale waliohitimu vyuo vikuu na wenye kampyuta na vifaa vingine vya teknolojia wanaweza kuvitumia kuwafundishia wanafunzi wakati wakisubiri Serikali kuboresha mazingira ya kufundishia.

Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Shule Direct, Iku Lazaro amesema wapo walimu ambao wana kompyuta kwenye mazingira ya kazi lakini hawawezi kuzitumia kutoa mafunzo na badala yake wanazitumia kopyuta hizo kuangalia filamu (series)

“Mwalimu amesoma chuo kikuu miaka mitatu na alikuwa anaitumia PC (kompyuta mpakato) yake kufanyia kazi za shule lakini akishaajiriwa, anaitumia kuangalia movies (filamu),” amesema Lazaro.

Mkurugenzi Mwanzilishi wa taasisi ya The Launchpad, Henry Kulaya amesema changamoto iliyopo katika elimu nchini, bado walimu hawajapewa uwezo wa kutosha wa teknolojia kuwarithisha wanafunzi wanaowafundisha. Picha| The Launchpad.

Lazaro amesema walimu wanasahau kuwa wanaweza wakaandaa “Slides” (maonyesho ya kompyuta)  ambayo yanaweza kufundisha wanafunzi wengi zaidi na kwa urahisi.

“Ukitumia projekta inakuwa rahisi kufundisha wanafunzi wengi kwa njia ambayo wanaifurahia kwani mwalimu mmoja kufundisha kundi la wanafunzi takribani 100 ni ngumu,” amesema Lazaro.


Zinazohusiana


Naye Mhadhiri wa taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Dk John Msumba amesema kuna haja mifumo ya elimu ya msingi na sekondari kuwa na uwezo wa kudhibiti waalimu ili kuhakikisha wanakuwa na ujuzi wa masuala ya tehama inayosaidia kwenye ufundishaji.

“Wapo wanafunzi ambao wanachukia kusoma somo fulani kwa sababu wanamchukia mwalimu ama namna anayofundisha,” amesema Dk Msumba.

Amesema endapo taasisi za elimu zitawafundisha wanafunzi wake kutatua changamoto mbalimbali hata kwa kuanzia ngazi ya shule zitawajengea wanafunzi uwezo wa kujifunza teknolojia ambazo zitawasaidia katika utendaji kazi wao.

Wadau hao wamesema ni vema Serikali iweke mkazo zaidi kuboresha miundombinu ya shule ili kuruhusu teknolojia kupenya kwa walimu na wanafunzi.