October 6, 2024

Wadau wataka mazungumzo kodi zinazosimamia kampuni zinazochipukia

Waishauri Serikali kuziangalia kampuni hizo kwa jicho la tatu ili kuzipa muda wa kujiimarisha kabla ya kuanza kutozwa kodi.

  • Waishauri Serikali kuziangalia kampuni hizo kwa jicho la tatu ili kuzipa muda wa kujiimarisha kabla ya kuanza kutozwa kodi.
  • Mabadiliko ya sheria na mazingira wezeshi ya biashara kuwaibua vijana wengi katika tasnia ya ubunifu wa teknolojia.

Dar es Salaam. Wadau wanaojihusisha na ujasiriamali wa teknolojia wameiomba Serikali kufikiria upya jinsi ya kuwasaidia kwa kuwatengenezea mfumo mzuri wa kulipa kodi ili kuondoa changamoto za usajili na ukuaji wa kampuni zinazochipukia ‘Startups’.

Hali hiyo inajitokeza wakati huu, katika kipindi ambacho vijana wengi wenye mawazo ya kibunifu wamekuwa na muamko wa kuanzisha kampuni za teknolojia ili kutatua changamoto mbalimbali zilizopo kwenye jamii.

Kampuni za teknolojia huchukua muda mrefu kutengeneza faida,  zinahitaji kulelewa na kutangazwa vya kutosha ili zijulikane sokoni na zinapokuwa zimesimama zinaweza kupewa kibali cha kuingia katika mfumo rasmi wa kodi.  

Hata hivyo, imekuwa changamoto kwao kukua na kuimarika kutokana na mfumo wa kodi  kuwajumuisha katika kundi moja la wafanyabiashara ambao wanatakiwa kulipa kodi bila kujali aina ya biashara wanayofanya.  

“Ukitaka kusajili kampuni TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) hasa hizi changa wenyewe hawana neno ‘Start Up’ wanakuona wewe ni mlipa kodi kama wengine,” amesema Nabiry Jumanne, mmoja wa waanzilishi wa mtandao wa Sheria Kiganjani unaotoa huduma za kisheria kupitia programu tumishi (App).  

Jumanne amesema kuwa ni wakati mwafaka kwa Serikali kuelewa kwa undani utendaji wa startups na kuwawekea mazingira wezeshi yatakayosaidia vijana wabunifu kuendeleza mawazo yao na baadaye walipe kodi.  


Zinazohusiana: 


Mfanyabiashara maarufu duniani ambaye anamiliki kampuni ya manunuzi mtandaoni ya  Alibaba,Jack Ma katika majukwaa tofauti ya amekuwa akizishauri Serikali za nchi za Afrika kuwapatia msamaha wa kodi wawekezaji wanaowekeza katika shughuli za ujasiriamali wa teknolojia mpaka aliwahi kushauri kuwa ili vijana hasa nchi za Afrika wanaowekeza kwenye ujasiriamali wa teknolojia mpaka pale watakopoweza kujiendesha kwa faida.

Edgar Mwampinge ambaye ni mjasiriamali wa teknolojia na mwanzilishi wa startup  ya Worknasi anafikiri Serikali ikae meza moja na wadau wa teknolojia ili kutoa mafunzo na namna nzuri ya kulipa kodi.  

“Mfumo wa kodi sio rafiki kwa aina ya biashara tunayofanya hasa katika teknolojia, wakati inachukua muda mrefu kuingiza pesa,” amesema Mwampinge.

Kampuni za teknolojia huchukua muda mrefu kutengeneza faida,  zinahitaji kulelewa na kutangazwa vya kutosha ili zijulikane sokoni na zinapokuwa zimesimama zinaweza kupewa kibali cha kuingia katika mfumo rasmi wa kodi. Picha|Mtandao.

Pamoja na changamoto hizo za kodi bado vijana wanajitoa kufungua kampuni zao ili waweze kujiajiri na kusaidia jamii katika kutatua matatizo katika sekta mbalimbali. 

Nao walezi wa startups wameiambia www.nukta.co.tz kuwa mabadiliko ya sheria hasa za kodi yatasaidia kampuni changa za teknolojia kupata uzoefu na tenda za miradi ya kibunifu zitakazosaidia kujiimarisha katika utengenezaji wa bidhaa na utoaji wa huduma bora zinazokidhi vigezo vya soko. 

“Ushauri ni kwa serikali kuwapa likizo ya kodi wajasiriamali wadogo/ startups kwa muda atleast(angalau)  mwaka mmoja wanapoanza ili wajenge msingi,” anasema Msimamizi Msaidizi wa kituo cha Buni Hub kilichopo chini ya Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Paul Madele.