Wagonjwa wa saratani wahakikishiwa tiba ya kisasa ya mionzi
Hilo limekuja baada ya Serikali kufanikiwa kuzindua jengo na mashine mpya za tiba ya mionzi ya ‘LINAC ambazo ni za kisasa.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipata maelezo juu ya mashine ya kisasa ya tiba ya saratani kwa mionzi kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road Dkt. Julius Maiselage wakati hafla ya uzinduzi wa Jengo na mashine za tiba ya saratani. Picha| Ofisi ya Makamu wa Rais.
- Hilo limekuja baada ya Serikali kufanikiwa kuzindua jengo na mashine mpya za tiba ya mionzi ya ‘LINAC ambazo ni za kisasa.
- Ameutaka Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) kwa kuingiza matibabu ya Saratani katika huduma ambazo wanagharimia ikiwemo tiba ya mionzi kwa LINAC.
Dar es Salaam. Katika kuimarisha huduma za upimaji na matibabu ya saratani nchini, Serikali imefanikiwa kuzindua jengo na mashine mpya za tiba ya mionzi ya ‘LINAC’ ambazo ni za kisasa.
Serikali imesema itaendelea kuimarisha huduma za saratani hasa huduma za kinga, uchunguzi na matibabu ya awali ikiwemo kuongeza vituo vya upimaji wa dalili za awali za saratani ya mlango wa kizazi na matiti ambapo mpaka sasa vituo 650 vinatoa huduma hiyo.
Akizundua jengo na mashine hizo jijini Dar es Salaam leo (Machi 29, 2019), Makamu Rais Samia Suluhu Hassan amesema tatizo la saratani kwa watanzania linaweza kupungua ama kuondoka endapo kutakuwa na tabia ya kupima afya mara kwa mara.
“Tunaweza kujikinga kwa kufuata kanuni za afya zinavyotuelekeza kula chakula bora, kufanya mazoezi mara kwa mara, na kuepuka kunywa pombe kupita kiasi na kuepuka matumizi ya tumbaku”alisema Makamu wa Rais.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, mradi wa ununuzi na ufungaji wa mashine mpya za kisasa za tiba ya mionzi umegharamiwa kwa asilimia 100 na Serikali ambapo mpaka kukamilika kwake imegharimu Sh9.5 bilioni.
Mama Samia amewataka wananchi wote hasa wanawake kufika katika vituo ili kufanyiwa uchunguzi kwani zikigundulika dalili za awali mgonjwa atatibiwa na kupona, huku akiwakumbusha wanaume kujitokeza kupima saratani ya tezi dume.
“Nashukuru wizara kwa kuanzisha kampeni ya upimaji wa virusi vya Ukimwi kwa wanaume, kwa kauli mbiu ya ‘Furaha Yangu’ na ingefaa suala hili liende pia kwa upimaji wa saratani ya tezi dume,” amesema mama Samia.
Soma zaidi: Teknolojia ya kisasa kuongeza ufanisi matibabu ya figo Muhimbili
Katika hatua nyingine, ameutaka Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) kwa kuingiza matibabu ya Saratani katika huduma ambazo wanagharimia ikiwemo tiba ya mionzi kwa LINAC.
Naye, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema katika kipindi kifupi cha miaka mitatu sekta ya afya imepata mafanikio makubwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo chanjo kwa watoto zimefikia asilimia 98, upatikanaji wa dawa muhimu ni asilimia 95, vifaa na vifaa tiba, huduma za mama na mtoto ikiwemo ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya.
Hata hivyo, amesema wanakusudia kukuza utalii kupitia sekta ya afya, “tumekusudia kuleta watalii wa matibabu.”