November 24, 2024

Waliolipia chaneli za bure watakiwa kuwasilisha taarifa zao TCRA

Hatua hiyo inakuwaja baada ya DSTV, AZAM TV na ZUKU kutii amri ya kuondoa chaneli za bure kwenye visimbuzi vyao.

  • Hatua hiyo inakuwaja baada ya DSTV, AZAM TV na ZUKU kutii amri ya kuondoa chaneli za bure kwenye visimbuzi vyao.
  • Taarifa hizo huenda zikasaidia kurejeshewa kwa pesa zao. 

Dar es Salaam. Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeanza kukusanya taarifa za wateja walionunua visimbuzi vya DSTV, Azam na Zuku na kulipia kutazama channeli za televisheni zisizo za kulipia, ambao miongoni mwao wamekuwa wakitaka kurudishiwa pesa zao.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na TCRA imeeleza kuwa watumiaji wote ambao walikuwa wanatozwa kutazama chaneli zisizo kulipia za TBC 1, ITV, STAR TV, CHANNEL TEN, EAST AFRICA TV na CLOUDS TV wanatakiwa kuwaslisha taarifa zao kwa mamlaka hiyo ili zifanyiwe kazi. 

Agost 7 mwaka huu TCRA iliziamuru kampuni za Multichoice Tanzania Limited (DSTV), Azam Media Limited (AZAM TV) na SimbaNet Tanzania Limited (ZUKU) kuondoa channeli za kutazamwa bila kulipia, baada ya kukiuka sheria na mashari ya leseni zao kwa kuwatoza watazamaji ada za viwango mbalimbali.

“Baada ya kutekeleza amri hiyo, sasa TCRA inakusanya taarifa za watazamaji waliotozwa ili kutazama chaneli hizi zisizo za kulipia hadi tarehe ya utekelezaji wa amri hiyo,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Wateja hao wanatakiwa kuwasilisha taarifa zenye jina la mtazamaji kama lilivyosajaliwa, aina kisimbuzi anachotumia, nambari ya kisimbuzi, nambari ya kadi ya kisimbuzi na eneo analoishi. Pia anatakiwa kuwasilisha kiasi cha pesa anacholipa kila mwezi na idadi ya miezi aliyolipia chaneli hizo za bure.


Zinazohusiana:


Taarifa hizo zinatakiwa ziifikie TCRA kwa barua pepe (e-mail) au barua ya kawaida kwenye anuani inayopatikana kwenye tovuti ya mamlaka hiyo.

Ikumbukwe kuwa Agosti 14 mwaka huu (2018), Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Makyembe aliingilia kati sintofahamu iliyojitokeza kati ya TCRA na kampuni za visimbuzi za DSTV, ZUKU na AZAM TV na kuzitaka zifuate sheria na miongozo ya leseni zao na  kuacha kufanya mambo kwa kujificha.

Pia alinukuliwa akisema wanaangalia uwezekano wa kupata ushauri kutoka kwa Mwanasheria wa Serikali namna ya kuwasaidia kurejeshea pesa watu ambao wamelipia chaneli za zisizo za kulipia.

Hatua ya TCRA kukusanya taarifa za watumiaji wa visimbuzi hivyo vitatu inakuja wakati kukiwa na malalamiko ya watu ambao wanadai kurudishiwa pesa zao walizolipia channeli za bure ambazo kwa sasa zimeondolewa katika visimbuzi vilivyotajwa.