October 6, 2024

Wanafunzi Chuo Kikuu wabuni teknolojia kuhifadhi bidhaa zinazoharibika haraka

Ni msaada kwa wafanyabiashara wa bidhaaa zinazoharibika mapema zikiwemo samaki.

  • Mashine hiyo ina uwezo wa kugandisha barafu kwa dakika kumi na kuokoa muda na umeme.
  • Ni msaada kwa wafanyabiashara wa bidhaaa zinazoharibika mapema zikiwemo samaki.
  • Serikali inaangalia iwezekano wa kuwawezesha kuendeleza ubunifu wao.

Dar es Salaam. Kwa mfanyabiashara, Praxeda Mathias suala la upatikanaji wa barafu kuhifadhi samaki ni muhimu ili kuwapatia huduma bora wateja wake.

Samaki hao anawasafirisha kutoka Ziwa Victoria Mwanza na kuwapeleka Jijini Dar es Salaam kwa kutumia gari lenye majokofu yanayotumia umeme wa gari kuhakikisha samaki wanafika salama kwa wateja.

“Biashara yangu inahitaji umeme na wakati mwingine hautulii hivyo hunilazimu kutafuta barafu ambazo zinakuwa ngumu kupatikana na  kupelekea baadhi ya samaki kuharibika,” anasema Mathias ambaye ana duka la samaki eneo la Boko wilaya ya Kinondoni. 

Majokofu hayo huenda sambamba na matumizi ya barafu ili kuhakikisha samaki wanaosafirishwa na kuhifadhiwa dukani hawaharibiki. Lakini changamoto ni upatikanaji wa barafu na kutumia muda mrefu kuganda kabla hazijaanza kutumika.

Kwa mujibu wa Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu Cha Illinois huko Urbana-Champaig, Marekani wamebaini kuwa jokofu la kawaida hutumia saa mbili hadi tatu kugandisha barafu ndogo ndogo. Wakati jokofu la kiwandani (Ice Maker) hugandisha barafu kwa dakika 90.

Kutokana na mchakato huo mrefu wa kugandisha barafu, ni changamoto kwa wasafirishaji wa samaki kama Mathias ambapo hulazimika kuingia gharama kubwa za kununua majokofu mengi ili kukidhi mahitaji ya barafu zinazohitajika kuhifadhi samaki na bidhaa zingine zinazoharibika haraka.  

Baadhi ya wafanyabiashara wa samaki wameiambia Nukta kuwa wamelazimika kufunga biashara zao kutokana na gharama kubwa za kutunza samaki ukilinganisha na faida ndogo wanayoipata. 

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Antony Mavunde (aliyevaa koti) akisikiliza maelezo kutoka kwa mwanafunzi Kelvin Lameck jinsi kifaa cha kusoma mita za maji kinavyofanya kazi, leo katika maonyesho ya miradi ya ubunifu, Mlimani City, Jijini Dar es Salaam.

 

Mvumilivu hula mbivu…

Licha ya changamoto ya uhifadhi wa samaki, bado Mathias ameendelea kuvumilia akisubiri uvumbuzi wa teknolojia mpya inayorahisisha upatikanaji wa barafu kwa muda mfupi. 

Changamoto hiyo imegeuka fursa kwa wanafunzi wawili wanaosoma katika Kitivo cha Uhandisi Umeme cha  Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph (SJUIT), Catherine Hole na Arnold Mgongo ambao wamevumbua mashine inayoweza kugandisha barafu kwa dakika 10.

Akizungumza leo katika maonyesho ya miradi ya ubunifu jijini Dar es Salaam, mwanafunzi Hole amesema mashine hiyo ina uwezo wa kufanya kazi kwa haraka kwa sababu inatumia maji chumvi ambayo huganda ndani ya nyuzi joto hasi 21 ( 21C) iliyo tofauti na maji ya kawaida (maji baridi) yanayoganda hadi nyuzi joto sifuri (0 C). Sawa na kusema maji chumvi yanapata baridi haraka lakini huchelewa kuganda ukilinganisha na maji ya kawaida.

Mashine hiyo imetengenezwa kwa kutumia kontena lenye mfano wa jokofu la kawaida, evaporeta, maji chumvi pamoja na mota.

                             

Jinsi teknolojia ya kugandisha barafu inavyofanya kazi. Video| Rodgers Raphael.

Mwanafunzi Mgongo amesema mashine hiyo haitumii umeme mwingi kwasababu barafu huganda kwa muda mfupi na hivyo kuwafaidisha wafanyabiashara wa bidhaa zinazotegemea barafu.

Akizungumzia teknolojia hiyo, Mfanyabiashara mwingine anayesafirisha samaki kutoka Mwanza kwenda Dar es Salaam, Tekla Buyamba ameishauri Serikali kuwawezesha vijana hao kuendeleza teknolojia hiyo ili iwafikie watanzania wengi wenye uhaba wa teknolojia ya utunzaji bidhaa zinazoharibika mapema.

“Kupatikana kwa mashine hii kunaweza kunisaidia kuongeza wateja kwa sababu samaki nitawasafirisha bila hofu ya kuharibikia njiani na hivyo itaninufaisha mimi na wateja wangu,” amesema Buyamba.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira na Walemavu, Antony Mavunde amesema Serikali inaangalia namna ya kuendeleza vipaji na ubunifu wa vijana wenye uthubutu ili wasaidia kuboresha hali ya jamii.