July 8, 2024

Wanaotikisa Twitter kwa hazina ya wafuasi wengi zaidi Tanzania

Rais Magufuli naye aingia katika 10 bora ya watu wenye wafuasi wengi Twitter miaka mitatu tangu ajiunge kwenye mtandao huo.

  • Rais Magufuli naye aingia katika 10 bora ya watu wenye wafuasi wengi Twitter miaka mitatu tangu ajiunge kwenye mtandao huo.
  • Wanawake wawili tu ndiyo waliopenya katika orodha hiyo.
  • Reginald Mengi aibuka kinara kwa kuwa na wafuasi wengi zaidi nchini.
  • Watu wenye wafuasi wengi mtandaoni huwa na ushawishi mkubwa katika jamii na hupata fursa ya kuwa karibu na idadi kubwa ya watu.

Dar es Salaam. Twitter limekuwa ni miongoni mwa mitandao ya kijamii ambayo miaka ya hivi karibuni imependwa kwa kasi  na kuwafikia watu wa kada mbalimbali ulimwenguni kama ilivyo kwa Facebook. Hadi kufikia mwanzoni mwa mwaka 2017 inakadiriwa kuwa watu milioni 330 walikuwa wakiutumia mtandao huo kwa mwezi.

Upekee wa mtandao huu wa Twitter ni uwezo wake wa kuchukua kuruhusu watumiaji kuandika maneno machache. Tofauti na Facebook au Instagram Twitter inaruhusu alama na herufi 140 tu na watumiaji wakuu wamekuwa ni watu maarufu kama wafanyabiashara, wasanii, wanasiasa, wanahabari, mashirika makubwa na vyombo vya habari.

Mtandao huu pia umekuwa kimbilio la wengi kuwasiliana na watu maarufu moja kwa moja kupitia uwanja wa wazi (Twitter feed) au kupitia meseji maarufu kama DM.

Nukta (www.nukta.co.tz) inakuletea orodha ya watu 10 maarufu wenye ushawishi na wenye wafuasi wengi katika mtandao wa Twitter kwa kutumia takwimu za mtandao wa takwimu za mitandao ya kijamii wa Socialbakers. Uchambuzi huo unahusisha takwimu za hadi Julai 24 2018. Sociabakers hutoa takwimu za watu na mashirika au kampuni mbalimbali zinazotumia mitandao ya kijamii. Takwimu hizo huchukuliwa kwa kutumia mfumo uliounganishwa moja kwa moja na mitandao husika. 

1. Reginald Mengi @regmengi 

Mfanyabiashara na Mwenyekiti wa Kampuni za IPP Limited anaongoza kwa kuwa na wafuasi 1.8 milioni. Hata hivyo, Mwandishi huyo wa kitabu kipya cha “I Can, I Must, I will”  anawafuata watu 19 pekee. Mara nyingi huwa anaandika vitu vinavyo washawishi vijana kufanya masuala ya ujasiriamali. Miaka ya hivi karibuni, Mengi alitumia ukurasa huo wa Twitter kuchochea mawazo ya kijasiriamali kutoka kwa vijana na alikuwa akiwapatia tuzo washindi.

2. Jakaya Mrisho Kikwete  @jmkikwete

Rais huyo mstaafu wa awamu ya nne Tanzania anashika nafasi ya pili kwa kuwa na wafuasi wengi katika mtandao huo  na amekuwa wa kwanza kwa wanasiasa kwa kuwa na jumla ya wafuasi milioni 1.1 huku akiwa anawafuata watu 44 tu. Kikwete aliyejiunga naTwitter Machi 2013, kwa sasa anatwiti sana masuala ya elimu, afya, watoto na wanawake na mara chache sana kuhusu maisha yake binafsi.

3. Zitto Kabwe Ruyagwa @zittokabwe 

Kwa watumiaji wa Twitter, hapana shaka wameshuhudia kuwa haiwezi kupita siku moja bila Zitto Kabwe kutwiti. Mbunge huyo wa jimbo la Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), anakamata nafasi ya tatu kwa kuwa na wafuasi zaidi ya 753,000 na nafasi ya pili kwa wanasiasa ambaye anaonekana ana ushawishi mkubwa kwa vijana wanaopenda siasa na wasiopenda siasa kwa mijadala anayoiibuka katika mtandao huo.


4. Diamond Platnumz a.k.a Chibu Dangote @diamondplutnumz

Mwanamziki huyo mashuhuri nchini katika akaunti yake binafsi ya Twitter ana wafuasi  574,520 na ikiwa ni theluthi tu ya  wale wanaomfuata Reginald Mengi. Hata hivyo, Diamond anakuwa msanii wa kwanza nchini kuwepo katika orodha ya wenye wafuasi wengi wa Twitter huku akizifuata akaunti 140 pekee.

5. Mohammed Dewji MO  @Moodewji

Mfanyabiashara mashuhuri nchini na mmoja wa mmiliki wa Timu ya mpira wa miguu ya Simba amekuwa ni mmoja wa mabilionea wenye ushawishi kwa vijana. Mo ambaye hutwiti mara kwa mara masuala ya biashara, uchumi, ushauri wa kijasiriamali na michezo hasa timu yake ya Simba anashika nafasi ya tano kwa kuwa na wafuasi zaidi ya 554,900 huku akiwa amewafuata watu 79 tu.

6. Halima James Mdee @halimamdee  

Halima Mdee moja ya wanasiasa wanawake mashuhuri nchini kutoka upinzani anakuwa mwanamke wa kwanza kuingia kwenye orodha ya watu wenye wafuasi wengi katika mtandao huo wa kijamii. Mdee ambaye ni Mbunge wa Kawe (Chadema) na Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) ana wafuasi zaidi ya 532,400.   Pia ndiye anayeongoza kwa kuwafuata watu wengi zaidi kati ya wale waliopo katika orodha ya 10 bora Twitter nchini baada ya kuzifuata. akaunti zaidi ya 10,200.

7. Jamii Forums  @jamiiForums

Mtandao wa Jamii Forums unaofahamika kwa mijadala moto mtandaoni kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii, kisiasa na utawala umeshika nafasi ya saba katika orodha ya watu au taasisi zinazofuatwa zaidi Twitter nchini. Ikiwa na wafuasi 526,700 Jamii Forums  ndiyo akaunti pekee inayohusiana na upashanaji habari iliyopenya katika orodha ya 10 bora wanaofuatwa Twitter. Pamoja na kuwa Jamii Forums hutegemea taarifa zaidi kutoka kwa watu na mashirika mbalimbali, bado ilikuwa inazifuata akaunti 530 tu.  

8. January Makamba @jmakamba

January Makamba ndiye Waziri pekee aliyeingia katika orodha hiyo ya akaunti bora zinazofuatwa zaidi Twitter. Makamba ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) wa Tanzania anashika nafasi ya nane baada ya kuweka kibindoni wafuasi 520,020 huku akifuata akaunti zaidi ya 2,800.

9. Salama Zalhata Jabir @AceJay

Mtangazaji mashuhuri Salama Jabir amebahatika kuwepo kwenye orodha hiyo ya dhahabu ya Twitter. Jaji huyo wa zamani wa Shindano la muziki la Bongo Star Search anashika nafasi ya tisa kwa kuwa na wafuasi wengi huku ni mtangazaji pekee aliyeingia katika orodha hii.  Salama aliyejipatia umaarufu mkubwa kupitia kipindi cha televisheni cha Planet Bongo, Bongo Star Search na Mkasi, anawafuata watu zaidi ya 1,050 huko akiwa anawafuasi zaidi ya 490,400.

10. Rais  John Magufuli @MagufuliJP   

Rais John Magufuli anashika nafasi ya 10 kwa watu wenye wafuasi wengi katika mtandao wa Twitter baada ya kujiunga nao Julai 2015.  Katika ukurasa huo uliothibitishwa na Twitter, Rais Magufuli ana wafuasi 445,000 huku akizifuata akaunti tisa tu. Kati ya akaunti tisa anazozifuata Rais Magufuli, akaunti nne ni viongozi wa nchi wakiwemo Rais wa Uganda Yoweri Museveni, Paul Kagame wa Rwanda na Uhuru Kenyatta wa Kenya. Rais Magufuli ndiyo mtu anayezifuata akaunti chache zaidi katika orodha hiyo. Mara nyingi Rais Magufuli hutwiti masuala mbalimbali ya maendeleo ya kitaifa.

Tafiti mbalimbali zinabainisha kuwa watu wenye wafuasi wengi mtandaoni wanaweza kuingiza kipato iwapo watahitaji kufanya hivyo kwa kusaidia kampuni au taasisi mbalimbali kufanya matangazo ya biashara mtandaoni.

Pia ni sehemu nzuri ya kurusha kampeni mbalimbali ili ziweze kufikiwa zaidi na watu. Watu maarufu wenye wafuasi wengi hutumia zaidi hii njia kuwafikia mashabiki wao na kusaidia jamii katika jambo fulani.

Hivi karibuni, kupitia mtandao wa Twitter, Mo Dewji na Waziri  Makamba walifanikisha kampeni ya kuchangisha pesa kwa ajili ya mwanafunzi wa udaktrari Arnold  anayesumbuliwa na ugonjwa wa figo. Katika kampeni hiyo, walifanikiwa kupata   takribani Sh30 milioni kwa kushirikiana na wadau wengine katika mtandao huo.