October 8, 2024

Wanayoweza kujifunza vijana wa Tanzania urejelezaji taka za kielektroniki Nigeria

Vijana wa Tanzania bado wana nafasi ya kujifunza kutoka kwa wenzao wa Nigeria ambao wameamua kuzibadilisha taka za kielektroniki yakiwemo mabaki ya kompyuta kuwa fursa ya kujiingizia kipato.

  • Baadhi ya vijana katika nchi ya Nigeria wameamua kuwa wabunifu na kugeuza taka hizo kuwa mali.
  • Vifaa vya taka hizo vinasafishwa na kuuzwa tena na visivyofaa vinaharibiwa au kuchomwa katika maeneo maalum ya kutupa taka hizo na kuwapatia kipato vijana hao.
  • Hii inaweza kuwa fursa kwa vijana wa Tanzania kutunza mazingira na kuokoa mazingira. 

Dar es Salaam. Vijana wa Tanzania bado wana nafasi ya kujifunza kutoka kwa wenzao wa Nigeria ambao wameamua kuzibadilisha taka za kielektroniki yakiwemo mabaki ya kompyuta kuwa fursa ya kujiingizia kipato. 

Shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), limesema taka za kielektroniki ni mbaya na hatari kwani haziyeyuki na zinachafua mazingira, lakini baadhi ya vijana katika nchi ya Nigeria wameamua kuwa wabunifu na kugeuza taka hizo kuwa mali.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN), katikati ya jiji la Lagos mji mkuu wa Nigeria taka za kielektoniki kwa miaka mingi zimekuwa ni changamoto kubwa kwa wakazi lakini sasa zinageuzwa kuwa thamani kwa kutumia mchakato mbadala wa kiuchumi.

“Lengo la mchakato huo ni kulinda mazingira na kutoa ajira salama kwa maelfu ya Wanigeria na hasa vijana,” inaeleza sehemu ya taarifa iliyotolewa na UNEP jana (Novemba 6, 2019). 

UNEP inaeleza kuwa kila mwaka, Nigeria inazalisha tani 290,000 za taka za kielektoniki pamoja na kupokea zaidi ya tani 70,000 za vifaa vilivyotumika vya kielektoniki kutoka katika mataifa yaliyoendelea.


Zinazohusiana: 


Lakini sasa vifaa hivyo vya elektroniki vikifikia mwisho wa matumizi yake na kutupwa vinakusanywa na vijana kutoka sekta isiyo rasmi na vifaa ambavyo bado vinaweza kutumika vinasafishwa na kuuzwa tena na visivyofaa vinaharibiwa au kuchomwa katika maeneo maalum ya kutupa taka hizo na kuwapatia kipato vijana hao.

Sekta hiyo ya kushughulika na taka za kielektroniki sasa inatoa ajira kwa watu zaidi ya 100,000 nchini Nigeria.

Hata hivyo, wataalam wa afya wanaonya kwamba kemikali za sumu zilizo katika taka za elektroniki zinasababisha madhara ya ngozi, matatizo ya kupumua, kupunguza maisha ya wanaoziharibu, kuchafua hewa, maji na udongo.

UNEP imesema kwa sasa Nigeria inaboresha sheria ya uwajibikaji kwa watengenezaji ili kuhakikisha wanawajibika na bidhaa wanazozalisha kwa muda wote wa mzunguko wa maisha ya bidhaa hizo.

Kwa mantiki hiyo, sekta salama na yenye ufanisi ya matumizi mbadala ina fursa kubwa kwa uchumi wa Tanzania, kwani vifaa hivyo vya elektoniki vilivyoharibika vina vitu vyenye thamani kubwa ndani yake kama dhahabu, madini ya platinum na vitu vingine adimu vya thamani.