November 24, 2024

Wanufaika wa Tasaf kupokea fedha kwa njia ya simu Tanzania

Ni baada ya Serikali kuanza mpango wa kuanzisha kanzidata ya wanufaika wa mfuko huo ili kuepusha changamoto zilizojitokeza hapo awali ikiwemo baadhi kupokea fedha mara mbili.

  • Ni baada ya Serikali kuanza mpango wa kuanzisha kanzidata ya wanufaika wa mfuko huo.
  • Wataanza kupokea fedha kwa njia ya simu ili kuepusha changamoto za kupokea fedha dirishani. 

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema imeanza mpango wa kuanzisha kanzidata ya kusajili wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) kwa kutumia Tehama na  wataanza kupokea fedha kwa njia ya simu ili kuepusha changamoto zilizojitokeza hapo awali ikiwemo baadhi kupokea fedha mara mbili.

Naibu Waziri wa Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deo Ndejembi ameliambia Bunge leo Februari 9, 2020 kuwa mpango wa kuanzisha kanzidata hiyo awali ulianza katika halmashauri 19 nchini lakini hadi sasa umefika katika halmashauri 39 na utaenda katika maeneo yote nchini.

Kiwango hicho cha halmashauri 39 zilizofikiwa na mfumo huo wa Tehama ni sawa na asilimia 21.1 au moja ya tano ya halmashauri za wilaya 185 zilizopo nchini. 

Mpango huo unaenda sambamba na kuweka mfumo utakaounganishwa na vitambulisho vya Taifa na mitandao ya simu ili kurahisisha utambuzi wa walengwa kupata fedha zao kwa wakati bila usumbufu. 

“Tayari tunaanza kuweka mfumo kwa ajili ya kuunganisha na NIDA (Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa) na mitandao yetu ya simu ili walengwa hawa badala ya kupokea fedha hizi dirishani kwa wale wanaoenda kugawa.

“Fedha hizi ziende moja kwa moja kwenye simu zao ili kuhakikisha kwamba hakuna double payment (malipo mara mbili) kwa sababu kuna maeneo ambayo watu wanalalamika mtu anapokea mara mbili au mtu akiwa hayupo wanachukua zile fedha,” amesema Ndejembi  jijini Dodoma.


Soma zaidi: 


Naibu waziri huyo alikuwa akijibu Swali la Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kagera, Neema Lugangira aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuanzisha kanzidata ya kuwasajili wanufaika wa Tasaf.

Miaka ya hivi karibuni Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika mifumo ya Tehama ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na ukusanyaji mapato ukiwemo mfupo wa GePG unaosaidia kukusanya mapato kupitia simu za mkononi. 

“Serikali ina mpango gani wa kuanzisha kanzidata kwa kutumia Tehama ili kuhakikisha kwamba wanaonufaika ni wale waliokidhi vigezo vilivyowekwa na kuondoa mianya ya watu wanaonufaika kusajiliwa mara mbili kwenye maeneo tofauti,” ameuliza Lugangira katika swali lake.

Kwa sasa Serikali inatekeleza awamu ya tatu ya Tasaf tangu mwaka 2012, ambayo itatekelezwa kwa miaka 10 mpaka 2023 katika vipindi viwili ambapo kipindi cha kwanza kilifikia ukomo mwaka juzi.

Serikali ilianzisha mfuko wa Tasaf mwaka 2000 kwa dhumuni la kuinua maisha ya kaya maskini Tanzania.