Wasaka pasipoti mpya za kielektroniki wazidi kumiminika Tanzania
Hatua ya Serikali kusitisha matumizi ya pasi za kusafiria za zamani mwezi uliopita imezidi kuongeza hamasa kwa Watanzania kutafuta nyaraka hizo na kufanya idadi ya wamiliki wa pasi mpya kufikia zaidi ya 300,000.
- Idadi ya watu waliopata pasipoti mpya za kielektroniki imefika 306,217 tangu zilizopoanza kutolewa Januari 31, 2018
- Serikali yasema haitaongeza muda wa matumizi ya pasipoti za zamani.
- Kenya yasogeza mbele muda wa kutumia pasipoti za zamani hadi Aprili 2021.
Dar es Salaam. Hatua ya Serikali kusitisha matumizi ya pasi za kusafiria za zamani mwezi uliopita imezidi kuongeza hamasa kwa Watanzania kutafuta nyaraka hizo na kufanya idadi ya wamiliki wa pasi mpya kufikia zaidi ya 300,000.
Idara ya Uhamiaji ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) leo kuwa hadi kufikia jana (Februari 25, 2020), idadi ya watu waliopata pasipoti mpya za kielektroniki imefika 306,217 tangu Januari 31, 2018 huku hamasa ya watu kuchangamkia fursa ya kupata hati hizo za kusafiria ikiwa ni ya kuridhisha.
Serikali ilisitisha rasmi matumizi ya pasipoti za zamani Januari 31, 2020 na haikuongeza tena muda mwingine huku ikiwataka ambao bado hawajabadilisha wafanye hivyo ili kupata fursa ya kusafiri nje ya nchi.
Mfumo wa utoaji pasipoti za kielektroniki ulizinduliwa na Rais John Magufuli Februari 1, 2018 ili kuchukua nafasi ya zile za zamani.
Msemaji wa Idara ya Uhamiaji Tanzania, Ally Mtanda amesema kati ya pasipoti hizo zilizotolewa, 303,788 au sawa na asilimia 99.2 ya pasipoti zote ni za kawaida (ordinary passport) huku waliopata pasipoti za utumishi wakiwa 517.
Waliopata pasipoti za kibalozi ni 1,907 na pasipoti maalum za kibalozi ni watano.
Pasipoti ya Utumishi (Service Passport) inaweza kutolewa kwa raia yeyote wa Tanzania ambaye yupo katika utumishi wa umma au anayeshika mamlaka ya ofisi kama ilivyoainishwa katika sheria ya pasipoti na hati za kusafiria namba 20 ya Mwaka 2002 na kanuni zake za mwaka 2004.
Idadi hiyo ya waliopata pasipoti mpya imezidi kungezeka ikilinganishwa na idadi ya watu 237,946 iliyoripotiwa na gazeti la The Citizen Januari 8, 2020. wiki tatu kabla ya kuzuia matumizi ya pasipoti za zamani.
Idara hiyo ilinukuliwa na gazeti hilo kuwa kwa miaka 10 kabla ya zoezi la kutoa pasipoti mpya, ni Watanzania 950,000 ndiyo walikuwa wanamiliki hati hizo ya kusafiria jambo linaloonyesha kuwa hadi sasa huenda bado watu wengi hawajafanikiwa kubadili pasi zao.
“Kumekuwa na maombi mengi kutoka nje ya nchi, lakini mikoani na hapa makao makuu bado tunaendelea kuhudumia watu, ingawa idadi siyo kubwa kabla hatujasitisha zoezi.
”Pasipoti hii mtu anaitafuta kwa madhumuni mbalimbali, mtu mwingine anatafuta pasipoti kama alikuwa ana issue (kazi) fulani, labda amesafiri mara moja haoni haja kuja kurenew (kuihuisha) ili akae nayo, lakini wale ambao ni wasafiri wa mara kwa mara hao wote washabadilisha pasipoti zao,” Mtanda ameiambia Nukta leo.
Soma zaidi:
- Kwanini kuna watumiaji wachache wa pasipoti katika huduma za kifedha?
- Sababu za kushangaza kuhusu rangi ya pasipoti yako
- Rwanda yazifuata Kenya, Tanzania kutoa pasipoti za kielektroniki
Mtanda amesema leo muamko wa watu kuomba pasipoti mpya za kielektroniki ni mkubwa lakini siyo kama uliokuwepo kabla ya kusitisha matumizi ya pasipoti za zamani Januari 31.
Ili kupata pasipoti mpya, mtu anatakiwa kulipa Sh150,000 na ataitumia kwa miaka 10, kabla ya kuihuisha tena.
Wakati Tanzania ikiwa imesitisha matumizi ya pasipoti za zamani, Kenya imesogeza mbele muda wa mwisho wa matumizi wa pasipoti hizo hadi Aprili 2021 wakati wakiendelea kutoa pasipoti za kielektroniki.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Kenya, Fred Matiang’i aliwaambia wanahabari Februari 24,2020 kuwa wamesogeza muda huo mbele kwa sababu Wakenya milioni 1.8 bado wanatumia pasipoti za zamani na wakizuiliwa watashindwa kusafiri na kupata huduma muhimu.
Mpaka sasa ni nchi nne katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) za Kenya, Tanzania, Rwanda na Uganda ndiyo zinatoa pasipoti za kielektroniki kwa raia wake.
Uamuzi wa kutumia pasipoti za kielektroniki zinazofanana ulifikiwa katika kikao cha 17 cha wakuu wa nchi wa jumuiya hiyo kilichofanyika Machi 2016 jijini Arusha.
Pasipoti za kielektroniki zinatajwa kuwa ni salama zaidi kuzitumia kwa sababu zimeunganishwa na mifumo ya usalama mtandaoni, jambo linalofanya iwe vigumu kwa mtu kuiba au kughushi taarifa za mtumiaji zilizopo katika kanzi data (data base).