October 6, 2024

Watanzania walivyoipokea huduma mpya ya sauti ya Vodacom Tanzania

Wamesema ni huduma nzuri hasa kwa watu wanaoishi mbali na maduka ya watoa huduma.

  • Ni “Sautipass” inayowawezesha watumiaji wa M-Pesa kutumia sauti zao kama nenosiri.
  • Baadhi wamehoji juu ya sheria inayomlinda mtumiaji pale atakapoibiwa kutokana na huduma hiyo.
  • Wengine wamesema itawasaidia watu wasioona kufanya miamala kwa urahisi. 

Dar es Salaam. Kila siku wabunifu wanabuni mifumo ya kidijitali inayorahisisha maisha ikiwemo mawasiliano kwa ajili ya kufanikisha shughuli za maendeleo.

Hivi karibuni, kampuni ya simu ya Vodacom Tanzania imeboresha programu yake inayotoa huduma za kifedha kwa njia ya simu ya M-Pesa kwa kuiongezea mfumo wa sauti unaowarahisishia watumiaji wake kuitumia. 

Vodacom imetambulisha “Sautipass”, mfumo unaomuwezesha watumiaji wa mtandao wakiwemo wenye ulemavu wa kuona kutumia sauti zao kama nenosiri wakati wa kutumia huduma hiyo badala ya kuandika.

Katika hatua za awali, “Sautipass” inamuwezesha mtu kurejesha akaunti ya M-Pesa iliyofungiwa na kubadilisha nenosiri bila kuhitaji kwenda kwa mtoa huduma. 

Meneja Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Alex Bitekeye amesema ili kutumia Sautipass, mtu anatakiwa kuisajili sauti yake ambayo atakuwa anaitumia kila anapoingiza nenosiri kwa sababu itakuwa imehifadhiwa ili kuepuka mtu mwingine kuingiza sauti yake. 

“Inashauriwa wakati unajisajili huduma ya Sautipass uwe katika mazingira tulivu na sauti iwe yako tu, ikitokea jogoo kawika kwenye sauti yako itahitaji jogoo huyo awike kila utakapokuwa unatumia huduma ya Sautipass,” amesema Biteyeke.

Amesema mfumo huo ni salama na hautohitaji mtu kusema namba zake za siri hadharani bali ni kuongea maneno yoyote na kisha mifumo ya Vodacom itang’amua sauti yake.

“Dunia inaelekea katika mifumo ya vitu visivyo na waya, kuondoa ulazima wa kushika, mifumo ya sauti kwa ajili ya miamala na kazi zingine. Ndiko dunia inakoelekea,” amesema Biteyeke huku akieleza huduma hiyo ni salama na ya uhakika kwa watumiaji wa M-Pesa. 

“Kwa namba ya siri, mtu anaweza kubashiri kwani kuna nafasi tatu za kuweka namba ya siri hivyo anaweza kuweka ya kwanza, ya pili na ya tatu akapatia, lakini hakuna mtu anayeweza kugeza sauti yako,” amebainisha. 

                   

Kwa mujibu Takwimu mpya za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), hadi kufikia Machi 2021 (robo ya kwanza ya mwaka huu) watumiaji wa huduma za kifedha kupitia simu za mkononi Tanzania wafikia milioni 32.7 na kati yao, asilimia 42 sawa na watu milioni 13.6 wanatumia huduma za Mpesa.

Wataalamu na wadau watoa maoni

Baada ya Vodacom Tanzania kutangaza huduma hiyo, Watanzania wametoa maoni yao huku baadhi wakisema huduma hiyo bado inaweza kuwa na changamoto ya usalama na wengine wakihoji sheria inayoendana na huduma hiyo.

Kwa Mkazi wa Shinyanga, Monica Meshack, huduma hiyo ni kama nyongeza kwake kwani hakupata changamoto katika huduma ya awali.

Amesema itarahisisha kwa ambao huwa wanasahau namba zao za siri au wanaolazimika kufunga akaunti zao za M-Pesa baada ya kuibiwa simu zao kupata huduma za kurudisha namba ya siri bila ulazima wa kwenda kwa watoa huduma.

“Kuna vijiji ambavyo viko mbali na maduka ya watoa huduma na huko ndiyo watu namba za siri huwa wanazisahau kutokana na kutokutumia M-Pesa zao mara kwa mara. Sautipass itawasaidia kurejesha namba zao za siri kwa urahisi bila haja ya kutembea umbali mrefu kupata huduma,” amesema Meshack.  

Wadau wa masuala ya teknolojia wamesema licha ya programu hiyo kuwa msaada kwa watu walio kwenye makundi la mahitaji maalumu hasa wasioona bado inaweza kuibua changamoto za kiusalama kwa watumiaji wake.

“Mfumo wa kuskani sura unaweza kudukuliwa kwa kupata picha ya mtu na kuelekezea sehemu ya kuskani, kwa sauti, mtu anaweza kurekodi sauti ya mtu na kuicheza na kupata huduma kwa urahisi lakini alama za vidole ni ngumu kufoji,” amesema mtaalam wa programu za kompyuta, Emmanuel Evance.

Mtaalamu huyo wa programu amesema kama angepata nafasi ya kuwashauri Vodacom, angeliwashauri kuwekeza zaidi katika mfumo wa alama za vidole kwani watu wengi kwa sasa wanatumia simu zinazoruhusu mfumo wa alama za vidole ambao ni salama zaidi.


Soma zaidi:


Hata hivyo, Mshauri wa masuala ya Dijitali wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited, Mihayo Wilmore amesema alama za vidole zinaweza pia kuwa na changamoto hasa ikizingatiwa Watanzania wengi wanafanya kazi za mikono na hivyo kuweka urahisi wa kufutika kwa alama hizo.

Kwa mtaalamu huyo wa masuala ya dijitali, huduma ya Vodacom siyo mpya na inatumika na nchi zingine ikiwemo Marekani kwa muda mrefu huku ikitajwa kuwa msaada kwa watu ambao hawaoni.

Wilmore amesema huduma hiyo ni nzuri kwani kisayansi mtu sauti yake hubadilika ndani ya miaka miwili na hivyo haitohitaji ulazima wa kusasisha sauti yako mara kwa mara. 

“Huduma hii (Sautipass) inarahisisha huduma, haikamilishi huduma. Kama ni kubadilisha neno siri la M-Pesa, utapiga simu maana yake namba yako inathibitishwa, utaongea kwa sauti yako, sauti inathibitishwa na utatumiwa pini yako,” amesema Wilmore.

Mdau huyo wa masuala ya teknolojia amesema licha ya kuwa teknolojia inaenda mbele, ni muhimu Vodacom kuzingatia kuwa baadhi ya sheria za Tanzania haziendani na mabadiliko yanayotokea kwenye sekta ya mawasiliano. 

“Hadi sasa sheria ya Tanzania haitambui mkataba ambao umesainiwa kidijitali kama mkataba kamili kama hakuna makubaliano ya wazi ya kutumia njia ya kidijitali. Sheria inatambua kidole gumba na saini ya wino,” amesema Wilmore.