November 24, 2024

Watumiaji wa simu wapungua kiduchu Tanzania

Wamepungua kwa asilimia 0.56 hadi kufikia milioni 43.7 Juni mwaka huu kutoka milioni 43.9 waliorekodiwa Machi 2019 ambapo kushuka kwa idadi hiyo kumechagizwa kushuka kwa idadi ya watumiaji wa makampuni matatu ya Tigo, TCCL na Zantel.

  • Wamepungua kwa asilimia 0.56 hadi kufikia milioni 43.7 Juni mwaka huu kutoka milioni 43.9 waliorekodiwa Machi 2019.
  • Kushuka kwa idadi hiyo kumechagizwa kushuka kwa idadi ya watumiaji wa makampuni matatu ya Tigo, TCCL na Zantel.

Dar es Salaam. Idadi ya watumiaji wa simu nchini Tanzania imepungua kwa asilimia 0.56 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2019, ikichagizwa zaidi na kushuka kwa wateja wa kampuni tatu zinazotoa huduma hiyo ya mawasiliano nchini. 

Uchambuzi  wa takwimu za robo ya pili ya mwaka 2019 (Aprili-Juni) zilizotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha kuwa idadi ya watumiaji wa simu imeshuka kidogo kutoka milioni 43.9  waliokuwepo Machi mwaka huu hadi milioni 43.7 waliorekodiwa Juni. 

Hiyo ni sawa na kusema watumiaji 247,497 au sawa na asilimia 0.56 waliokuwepo Machi 2019 hawapati tena huduma hizo za mawasiliano. 

Hata hivyo, iwapo watumiaji hao watapimwa ndani ya robo ya pili pekee yaani kati ya Aprili hadi Juni, takwimu hizo za TCRA bado zinabainisha kuwa idadi yao ilipungua kwa watumiaji 125,247. 

Matumizi ya simu hupimwa kwa idadi ya watu waliojisajili kutumia mitandao ya simu za mkononi inayotoa huduma hiyo nchini ikiwemo ya Vodacom, Tigo, TCCL, Zantel, Halotel, Smile na Smart.

Kushuka kwa idadi hiyo kumechagizwa na makampuni matatu ya Tigo, TTCL na Zantel ambayo yamepoteza wateja kwa viwango tofauti katika kipindi hicho.

Kampuni iliyopoteza wateja wengi ni Tigo ambayo mwezi Machi ilikuwa na watumiaji milioni 12.5 lakini wamepungua hadi milioni 11.6 Juni mwaka huu.

Kwa muktadha huo, Tigo imepoteza watumiaji 798,282  hadi kufikia Juni mwaka huu na kuchangia kwa sehemu kubwa kushuka kwa idadi ya jumla ya watumiaji wa simu Tanzania. 

Hata hivyo, takwimu za TCRA zinaonyesha kuwa dalili za Tigo kupoteza wateja zilianza kuonekana tangu Januari ambapo kwa miezi sita mfululizo ya nusu ya kwanza ya mwaka huu idadi ya wateja wake imekuwa ikiporomoka kwa viwango tofauti. 

Januari ilikuwa na watumiaji milioni 12.6 kabla hawajushuka hadi kufikia milioni 12.4 mwezi Machi na kuporomoka zaidi hadi milioni 11.6 Juni mwaka huu.

 Wakati kampuni hizo tatu zikipoteza baadhi ya wateja wake, kampuni za Vodacom, Airtel, Halotel zinafanya vizuri, kwa mujibu wa takwimu za TCRA, idadi ya watumiaji wake imekuwa ikiongezeka. Picha|Daniel Samson.

Shirika la mawasiliano ya simu Tanzania (TCCL) nalo limepoteza wateja 120,818 ambapo Machi ilikuwa na watumiaji 801,163 kabla hawajapungua hadi kufikia 716,206 Juni mwaka huu.

Licha ya kuwa watumiaji wa TCCL kupungua kipindi hili bado imekuwa na mwenendo wa kupanda na kushuka kwa watumiaji wake.

Mathalan, Aprili ilikuwa na watumiaji 837,024 lakini mwezi uliofuata wakapungua hadi 673,363 kabla ya kuongezeka hadi 716,206 mwezi Juni mwaka huu. 

TCCL ambayo hadi kufikia Machi mwaka huu ilikuwa inamiliki asilimia mbili ya soko la simu Tanzania, rekodi ambayo iliivunja Desemba 2018 sasa imerudi tena kwenye asilimia moja iliyoishikilia kwa miaka nane iliyopita. 

Katika siku za hivi karibuni, Serikali imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali ikiwemo kuipatia fedha TCCL ili ifanye vizuri na kuhimili soko la ushindani dhidi ya makampuni mengine kama Vodacom ambayo inashikilia theluthi ya soko lote la mawasiliano Tanzania. 

Kampuni nyingine ambayo watumiaji wake wamepungua ni Zantel. Katika robo ya kwanza ilikuwa na wateja milioni 1.21 ambao wamepungua kutoka milioni 1.22 waliokuwepo robo ya pili mwaka huu. 

Wakati kampuni hizo tatu zikipoteza baadhi ya wateja wake, kampuni za Vodacom, Airtel, Halotel zinafanya vizuri, kwa mujibu wa takwimu za TCRA, idadi ya watumiaji wake imekuwa ikiongezeka. 

Watumiaji wa Vodacom na Halotel katika robo ya pili wameongezeka kwa asilimia moja mtawalia. 


Soma zaidi:


Hata wakati, kampuni hizo tatu zikipotez awateja, watumiaji wa jumla wa simu wamekuwa wakishuka na kupanda kwa nyakati tofauti. 

Mathalani, mwezi Machi Tanzania ilikuwa na watumiaji wa simu milioni 43.9, wakashuka hadi milioni 43.8 mwezi uliofuata kabla hawajaporomoka zaidi hadi milioni 43.5 mwezi Mei. 

Hata hivyo, mambo yakabadilika mwezi uliofuata wa Juni ambapo idadi ikaongezeka hadi kufikia watumiaji milioni 43.7 sawa na ongezeko la watumiaji 198,826.  

Nini sababu ya kushuka kwa watumiaji?

Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha kunakuwa na matumizi sahihi na kudhibiti utitiri wa laini za simu, jambo lililosaidia kupunguza vitendo vya udanganyifu na wizi mtandaoni. 

Machi 1, 2018 mfumo wa kusajili laini kwa kutumia laini za vidole (Biometric Registration) ulizinduliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)  baada ya kuwapo vitendo vya watumiaji wa huduma hiyo kugushi vitambulisho au kutumia vitambulisho vya watu wengine.

Msisitizo umewekwa zaidi mwaka huu ambapo TCRA wanatekeleza mfumo huo kwa kushirikiana na watoa huduma za simu za mkononi na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida).

Hata hivyo, Nukta haikuweza kupata kwa wakati majibu ya TCRA juu ya sababu zilizosababisha watumiaji wa simu nchini kushuka katika kipindi hicho.