October 8, 2024

Wazazi wanavyoweza kuwasaidia wanafunzi kusoma wakiwa nyumbani

Kipindi wazazi wana kila sababu ya kuhakikisha watoto wao wanaendelea kuelemika kwa njia tofauti wakiwa nyumbani ili waweze kutimiza ndoto zao kielimu.

  • Ni pamoja na kuwatengenezea ratiba ya masomo watoto.
  • Pia watoto wapewe nafasi ya kucheza na kupumzika.
  • Kwa wanavyuo, wameshauriwa kuomba miongozo ya masomo kutoka kwenye vyuo vyao ili kusoma kwa njia ya mtandao.

Dar es Salaam. Licha ya shule za msingi, sekondari na vyuo kufungwa kuepuka maambukizi ya virusi vya Corona, wadau wa elimu wameshauri mambo ambayo wazazi wanaweza kufanya kwa watoto wao ikiwemo kuwatengenea muda kwa ajili ya kusoma masomo ya darasani. 

Serikali ya Tanzania imefunga shule na vyuo vyote nchini na wanafunzi wametakiwa kukaa nyumbani kwa siku 30 ikiwa ni hatua ya kupunguza mikusanyiko ya watu na kujikinga na Corona. 

Kipindi wazazi wana kila sababu ya kuhakikisha watoto wao wanaendelea kuelemika kwa njia tofauti wakiwa nyumbani ili waweze kutimiza ndoto zao kielimu. 

Verediana Mwashi ni mkazi wa jijini Dar es Salaam na mama wa watoto watatu ambao kwa sasa wote wapo nyumbani. 

Mwashi amesema mbali na kuwakazania watoto wake wajisomee, bado anatafuta mbinu zingine za kuwasaidia watoto wake wasibweteke kielimu.

“Wakiamka wanaoga, wanakunywa chai na kisha wanaingia kusoma. Watasoma hadi muda wa chakula cha mchana ndiyo watapata nafasi ya kucheza,”amesema Mwashi.

Huenda upo kwenye nafasi kama Mwashi kiasi cha kuumiza kichwa ni kwa njia gani utawasaidia watoto wako wasome. Hizi ni njia ambazo Nukta (www.nukta.co.tz) imezichambua kwa ajili yako.

Vipindi vya televisheni na video za Youtube

Verediana amesema watoto wake wanapenda kushika simu yake na mara nyingi huingia kwenye app ya “Youtube kids” ambayo ni mahususi kwa video za burudani na mafunzo ya watoto. 

Wakati watoto wakijihisi wanajiburudisha kwa kutazama video za mafunzo, mara nyingi wanakuwa wanajifunza pasipo wao kujua.

“Janelle akishika simu yagu anaingia YouTube na anatafuta mafunzo ya alfabeti na namba. Imemsaidia kwenye kumjengea uwezo wa masomo ya hisabati na lugha,” amesema mama huyo akimuelezea mtoto wake wa mwisho mwenye miaka minne.

Kama una televisheni nyumbani, chaneli ya TBC inaonyesha kipindi cha “Akili and Me” ambacho kinafundisha mambo mbalimbali yakiwemo maarifa ya jamii, jinsia na hata hesabu na sayansi.

Kwa kupitia mafunzo yaliyopo kwenye mitandao kama Youtube, watoto huburudika na kujifunza pasipo kujua.Picha| Ozobot.

Kuwapangia na kuifuatilia ratiba ya kujisomea 

Unaweza kuwapatia jukumu la kuandaa ratiba na kisha kuipanga upya kwani hakika masomo magumu wanaweza kuyaweka mwishoni. 

Mwalimu wa watoto anayejitegemea, Glory Mushi amesema mzazi anaweza kuwasaidia kuandaa ratiba ya masomo kuhakikisha kuwa wanafuatilia kila somo ambalo wanafundishwa shuleni.

Kumbuka wakirudi shuleni watakimbizwa. Watakuwa nyuma kwahiyo wazazi wanahitaji kuhakikisha watoto wao wapo kwenye njia sahihi.

Kama mzazi hana ufuatiliaji, itakuwa ni mbaya kwa watoto,” amesema mwalimu Mushi.

Kutenga chumba kwa ajili ya kujisomea

Moses Raymond ambaye ni baba wa watoto watatu amesema ni muhimu kutenga chumba cha watoto kujisomea na kuhakikisha uwepo wa vitabu na intaneti kwa ajili yao.

Zaidi ni muhimu mzazi kufuatilia maendeleo ya kujisomea kwao.

Kutenga chumba au nafasi kwaajili ya kujisomea itasaidia mtoto wako kukazania masomo na kuepukana na vizuizi vikiwemo televisheni na kelele za watu waliopo nyumbani.

Raymond pia ameungana na Glory kwenye kuandaa ratiba ya kujisomea na siyo kujisomea kiholela.

Lakini watoto wapate nafasi ya kucheza na kupumzika vizuri na kufanya shughuli ndogo ndogo za nyumbani.


 Zinazohusiana


Hayo yote ni kwa wanafunzi wa sekondari na shule za msingi. Vipi hali ya wanachuo inakuwaje?

Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Tumaini kampasi ya Dar es Salaam (Turdaco) Idara ya Sanaa na Sayansi Jamii MaryHospicia Kafyome amesema hali ni ngumu kwa wanafunzi wa vyuoni kwani wengi wamemaliza mhula na mitihani wameshafanya.

Kafyome amesema ni vigumu kujisomea pasipokuwa na muongozo wa kozi kwani wanafunzi wengi hawana miongozo hiyo.

Hata hivyo, amewasihi wanafunzi wa vyuoni kuomba miongozo hiyo na kuanza kujisomea kwa njia ya mtandao wakisubiri kurejea vyuoni.

“Ni changamoto kubwa ni kwamba hawana course outlines (Miongozo ya kozi) labda kuomba kwenye idara course outlines ili waanze kujisomea,” amesema Kafyome.