October 6, 2024

WhatsApp yafuata nyayo za Facebook matangazo ya kibiashara

Mtandao huo umetangaza kuwa utaanza kuweka matangazo ya kibiashara katika kurasa zake ifikapo 2020.

WhatsApp yaja kivingine yaanza kutumia matangazo kujiingizia kipato. Picha|Mtandao.


  • Mtandao huo umetangaza kuwa utaanza kuweka matangazo ya kibiashara katika kurasa zake ifikapo 2020. 
  • Matangazo hayo yataanza kuonekana kwenye “Status stories”.

Dar es Salaam. Hatimaye Mtandao wa WhatsApp umechukua hatua mpya ya kujiingizia kipato, baada ya kutangaza kuanza kupokea matangazo ya kibiashara kuanzia mwaka 2020.

Mtandao huo umbao uko chini ya umiliki wa Mwanzilishi wa Facebook, Mark Zuckerberg utaanza kuweka matangazo hayo kwenye ‘status stories’ ili kuwafikia watu wengi kirahisi. 

Taarifa ya WhatsApp kujitosha katika matangazo ya kibiashara kama ilivyo kwa Facebook na Instagram imetolewa katika Mkutano wa mwaka wa Masoko wa Facebook nchini Uholanzi.

Katika kufanikisha hilo mtandao huo wenye watumiaji wapatao bilioni 1.5 ulimwenguni utaongeza kitu kipya ifikapo mwaka 2020 ambapo kupitia matangazo ya ndani ya WhatsApp ( WhatsApp’s ‘Status-stories’) wataanza kuweka  matangazo katika eneo la hilo.

Eneo lingine la matangazo litakuwa kwa ajili ya program tumishi za Facebook ambapo kutakuwa na matangazo yanatoka Facebook ( Ads that click to WhatsApp (FB)) na Instagram (Ads that click to WhatsApp (IG)) ambapo mtu akibofya atapelekwa moja kwa moja kwenye App ya WhatsApp.


Zinazohusiana:


Ingawa tangu kutoka kwa tangazo hilo kumekuwa na malalamiko na maoni tofauti kwa watumiajie wake ulimwenguni ambapo baadhi yao wamesema uhuru wao utapungua kwa sababu ya matangazo hayo.

Tangu kuanzishwa kwake mtandao huo,  waanzilishi wake,  Brian Acton na Jan Koum waliwaambia watumiaji wake kuwa hataruhusu mfumo wa mtangazo ambapo watumiaji wa mtandao huo awali walikuwa wanachangia senti 99 dola za kimarekani kwa mwaka kwa ajili ya uanachama.

Hata hivyo, tangu mtandao huo uliponunuliwa na Facebok mwaka 2014 kwa gharama ya dola za Marekani 19 bilioni watumiaji wake wamekuwa hawatozwi tena pesa ili kutumia mtandao huo.