October 6, 2024

WhatsApp yaja na maboresho mapya kwa wafanyabiashara

Imeboresha programu yake ya “WhatsApp Business” kwa kuongeza kipengele kipya kitakachowawezesha wafanyabiashara kuweka taarifa muhimu za bidhaa na huduma.

  • Imeboresha programu yake ya “WhatsApp Business” kwa kuongeza kipengele kipya kitakachowawezesha wafanyabiashara kuweka taarifa muhimu za bidhaa na huduma.
  • Kipengele  hicho kinaongeza wigo wa masoko na ukaribu na wateja wao.
  • Wadau wasema ni hatua muhimu kukidhi mahitaji ya wafanyabiashara. 

Wafanyabiashara wanaotumia programu tumishi ya simu (app) ya WhatsApp Business, sasa wana kila sababu ya kutabasamu kwa sababu programu hiyo itawasogeza karibu zaidi na wateja wa bidhaa na huduma wanazotoa. 

Programu hiyo inayoendeshwa na mtandao wa WhatsApp imeongezewa kipengele kipya kitakachowawezesha wafanyabiashara kuweka taarifa muhimu za bidhaa na huduma zao ikiwemo picha wakati wowote. 

Hatua hiyo inawaondolea changamoto iliyokuwepo awali ya kukosa uwanja mpana wa kuwasiliana na wateja wao, jambo lililowafanya wapoteze baadhi ya fursa muhimu za masoko katika biashara zao. 

Kwa kupitia kipengele hicho, mteja atapata taarifa za bidhaa na huduma kwa undani, hata pasipo kwenda katika tovuti au mitandao mingine ya muuzaji.

Taarifa iliyotolewa na WhatsApp  inaeleza kuwa mfanyabiashara atakuwa na uwezo wa kuweka taarifa hizo kwa kufungua app ya WhatsApp Business na kuingia kwenye kipengele cha mpangilio (Settings) kisha mpangilio wa biashara na mwisho kuingiza taarifa zote anazohitaji kuweka kwa ajili ya wateja wake. 

“Mpangilio wa biashara ni muhimu kwa ajili ya wateja kwa sababu huonesha taarifa zote muhimu zinazohitajika na mteja kutoka kwa mfanyabiashara kama picha za bidhaa na taarifa zote za bidhaa husika”, inasomeka sehemu ya taarifa hiyo iliyotolewa Novemba 7, 2019.


Zinazohusiana:


Hata hivyo, huduma hiyo inayopatikana katika simu za Android na IPhone imeanza kutumiwa na wafanyabiashara wa Brazil, Germany, India, Indonesia, Mexico, Uingereza na Marekani na itasambaa katika maeneo mengine duniani hivi karibuni. 

Mtumiaji wa app hiyo, Adam Sembaya amesema mabadiliko hayo yatawasaidia wafanyabiashara kwa sababu, ni ngumu kutuma picha kwa kila mteja anayemwandikia meseji badala yake wakiweka utaratibu wa kupangilia taarifa za bidhaa itakuwa rahisi zaidi kwa wateja.

“Kuna wakati unakuwa umetingwa sana, meseji zinakuwa nyingi hivyo, inakuchukuwa muda kumpa kila mteja taarifa zinazohitajika. Utaratibu huo utatusaidia mno aisee,” amesema Adam.