November 24, 2024

Youtube yawaonya wazalishaji wa maudhui kwenye mtandao wake

Youtube imeahidi kuondoa maudhui yoyote yatakayokuwa na chembe za kukiuka vigezo na masharti yao.

  • Youtube imeahidi kuondoa maudhui yoyote yatakayokuwa na chembe za kukiuka vigezo na masharti yao.
  • Itasaidia katika kuandaa watengeneza maudhui walio makini na kukuza soko la mtandao.

Wakati mtandao wa Youtube ukiendelea kukuza na kuendeleza biashara za watumiaji lukuki wa mtandao huo, bado umeonekana kutoridhishwa na viwango vya uwajibikaji vya watumiaji na kuwaonya kuwa sasa itakaza uzi katika kudhibiti maudhui yanayokiuka vigezo na masharti.

Mkurugenzi Mtendaji wa Youtube, Susan Wojcicki katika salamu zake kwa watumiaji amesisitiza matumizi mazuri ya mtandao kwa kuzingatia masharti yaliyopo.

Miongoni  mwa masharti hayo ni pamoja na kutopakia maudhui yanayopingana na sheria za ndani ya nchi yako na kuhakikisha kila maudhui yanachapishwa yana tija na kuwapa uhuru watu kutoa maoni juu yake.  Pia, Youtube hairuhusu kuchapishwa kwa maudhui ya ngono ambayo ni marufuku karibu katika mataifa yote ulimwenguni. 

Kuzingatia vigezo na masharti ni muhimu kwajili ya kukuza mtandao huo.Picha| Mtandao.

Youtube imeahidi kuondoa maudhui yoyote itakayokuwa na chembe za kukiuka vigezo na masharti vilivyowekwa na mtandao huo kwa lengo kubwa la kutunza hadhi ya jukwaa hilo linalofikia mamilioni ya watu katika nchi mbalimbali ulimwenguni.  

Hata hivyo, amesema wataendelea kutoa zawadi kwa wazalisha bora wa maudhui kwa kuwa ni moja ya sababu zinazofanya mtandao huo kufanya kazi kwa weledi. 

“Pamoja na hayo, lengo kuu la jukwaa ni kuandaa watengeneza maudhui makini, hivyo ni muhimu kwa wao kutia moyo wale wanaofanya vizuri kulingana na wanacholisha jamii inayowazunguka,” amesema Wojcick.

Youtube imekuwa ni chachu ya kukua kwa biashara mbalimbali ulimwenguni ikiwemo Tanzania na kusaidia kutengeneza kipato kikubwa kwa wazalishaji maudhui na wafanyabiashara wanaotangaza katika mtandao huo.


Zinazohusiana:


Wasanii na wanahabari nchini ni miongoni mwa wanufaika wakubwa wa mtandao huo baada ya kuwa chanzo kizuri cha mapato. 

Pia, Youtube imekuwa msaada wa upatikanaji wa maudhui ya televisheni kirahisi tofauti na miaka ya nyuma ambapo mtu alihitaji kuwa na vifaa vingi vya kielektroniki kupata huduma hizo.