July 8, 2024

Zijue tovuti unazoweza kusoma bila intaneti Tanzania

Kampuni ya mawasiliano ya simu ya Vodacom Tanzania imetoa orodha ya tovuti tisa za elimu na taarifa ikiwemo ya Wizara ya Afya ambazo wateja wake wanaweza kuperuzi bila malipo yoyote ya vifurushi vya intaneti.

  • Ni tovuti za elimu na taarifa ambazo unaweza kuingia kwa kutumia laini ya Vodacom.
  • Zitawasaidia wanafunzi na wananchi kujielimisha wakati huu wa mlipuko wa Corona.
  • Vodacom yasema inawapunguzia gharama za intaneti watumiaji wa mtandao huo.

Dar es Salaam. Kutokana na umuhimu wa upatikanaji wa elimu na taarifa, kampuni za teknolojia na wabunifu wanaendelea na jitihada za kuwawezesha Watanzania kupata taarifa muhimu kuondoa ujinga kwa kutumia simu na kompyuta kwa kuondoa maumivu makubwa ya kifedha.  

Kampuni ya mawasiliano ya simu ya Vodacom Tanzania imetoa orodha ya tovuti tisa za elimu na taarifa ikiwemo ya Wizara ya Afya ambazo wateja wake wanaweza kuperuzi bila malipo yoyote ya vifurushi vya intaneti. 

Hiyo ina maana kuwa mtu anayetumia laini ya Vodacom anaweza kuingia katika tovuti hizo na kusoma mambo anayoyataka bila kukatwa bando lake hata kama hana intaneti kwenye simu.

Vodacom Tanzania imezitaja tovuti za elimu za SmartClass, DIT E-Learning, SmartClass Africa, Shule Direct, mfumo ujifunzaji wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Learning Management System) na Instant School inayomilikiwa na kampuni hiyo.

Tovuti hizo zimekuwa zikiwasaidia wanafunzi kujifunza masomo ya darasani mtandaoni wakiwa nyumbani hasa kipindi hiki ambacho hawawezi kwenda shuleni kwa sababu ya tahadhari ya ya kujikinga na ugonjwa wa virusi vya Corona. 


Soma zaidi: 


Tovuti tatu zilizobaki ni za Serikali za Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Idara ya Habari-MAELEZO. 

Zimekuwa zikitumika kutoa taarifa mbalimbali hasa zinazohusu Corona na tahadhari ambazo wananchi wanatakiwa kuchukua kujikinga na ugonjwa huo. 

Hata hivyo, huduma hiyo ya Vodacom zitawafaa zaidi watu wenye simu janja na kompyuta zinazoweza kuunganishwa na intaneti. 

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Hisham Hendi ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa  wameamua kutoa huduma hiyo baada ya kupokea maombi mengi kutoka kwa wanafunzi na vyuo ya kupunguza gharama za intaneti. 

Amesema njia sahihi ya kuwapunguzia gharama ni kuwawekeza tovuti hizo muhimu ambazo wanaweza kuperuzi na kupata taarifa na elimu bila makato ya intaneti.