Zingatia haya wakati ukitumia vifaa vya kielektroniki jikoni
Ni kweli jokofu limetengenezwa kwa ajili ya kuhifadhi vyakula ili visiharibike na ni kweli kifaa cha kupashia vyakula (Microwave) kimenunuliwa kikiwa na nafasi ya kupasha mlo mmoja kwa wakati mmoja. Lakini vinahitaji ubunifu kuvitumia kwa faida.
- Unaweza kuandaa vizuri vyakula vyako kabla ya kuweka kwenye jokofu ili kuepuka kazi ya kuviandaa tena wakati wa kutumia.
- Pia unaweza kupasha milo miwili tofauti kwenye “microwave” kwa wakati mmoja.
Ni kweli jokofu limetengenezwa kwa ajili ya kuhifadhi vyakula ili visiharibike na ni kweli kifaa cha kupashia vyakula (Microwave) kimenunuliwa kikiwa na nafasi ya kupasha mlo mmoja kwa wakati mmoja.
Lakini, mambo haya yanahitaji ubunifu ili kuhakikisha umeme wako haupotei na kukuongezea gharama zisizo za lazima.
Baada ya kukuletea makosa ambayo umekuwa ukiyafanya wakati wa kutumia simu yako ya mkononi, haya ni mambo machache unayoweza kuyafanya ili kurahisisha maisha yako wakati ukitumia kwa vifaa vyako vya jikoni:
Matumizi sahihi ya vifaa vya kielektroniki wakati wa maandalizi wa chakula jikoni, ndiyo njia sahihi ya kuvifanya vidumu na vikusaidie kupata matokeo unayotaka. Picha| Naomi Hébert/Unsplash.
- Viandae vyakula vizuri kabla ya kuhifadhi kwenye jokofu
Huenda wewe ni kati ya wadau ambao wakienda sokoni kununua mahitaji ya nyumbani, wakirudi huhifadhi vitu hivyo bila hata kuviosha.
Ni kwanini upate tabu ya kuloweka mboga zako baada ya kuzitoa kwenye jokofu la kugandisha? Ni busara kuziandaa mboga zako kabla ya kuzihifadhi kwenye jokofu ili ukizitoa kwenye jokofu safari inakuwa ni moja tu ya kuweka kwenye sufuria na kupika.
Kwa kufanya hivi, utarahisisha kazi yako jikoni hasa kwa mikono kupata ganzi wakati wa kushika barafu na mboga zilizoganda.
- Pasha milo miwili kwa wakati mmoja kwenye “Microwave” yako
Ndiyo! inawezekana. Wakati wengi wakishindwa kupasha milo miwili kwa wakati mmoja kwenye kifaa hiki, jambo ambalo linapelekea chakula ambacho kimepashwa mara ya kwanza kupoa wakati kingine kinaendelea kupashwa, fahamu kuwa unaweza kupasha milo miwili kwa mkupuo.
Unachohitaji ni bakuli moja, sahani moja na kikombe. Tanguliza bakuli yenye chakula na kisha weka kikombe ambacho juu yake utaweka sahani yenye chakula kingine. Ni rahisi namna hiyo.
Sasa unaweza kupasha chakula chako na cha mgeni wako kwa wakati mmoja.
Zinazohusiana
- Makosa unayotakiwa kuepuka wakati unatumia simu yako
- Mbinu tano za kudhibiti matumizi makubwa ya intaneti kwenye ‘smartphones’
- Siyo kila chakula ni cha kugandisha
Watumiaji wengi wa majokofu hawafuatilii kiasi cha ubaridi kinachofaa kwenye chakula fulani. Wengi hujikuta wakigandisha hadi matikiti maji wakidhani yatakua sawa baada ya kuyatoa kwenye jokofu.
Kwanini uhangaike, baadhi ya vyakula hupoteza ladha vikigandishwa na endapo utavitumia baadaye, hautafurahia ladha yake.
Vyakula kama matikiti na matunda mengine yenye maji mengi havifai kugandisha badala yake vinahitaji ubaridi wa wastani tu. Kama huna utaalamu wa kiasi cha ubaridi na chakula, unaweza kumuomba kijana wako au mtaalamu mwingine akusaidie kuweka ubaridi utakaofaa kwa vyakula vyako kwenye jokofu.
Siyo kila tunda au mboga inafaa kuwekwa kwenye jokofu. Angali zile ambazo unaweza kuhifadhi mahali salama ili zisiharibike. Picha| Ayda Oz/Unsplash
- Gandisha viungo vyako na mafuta
Umewahi kununua viungo “fresh” kama gilihiliani, vitunguu maji na vinginevyo ambavyo huharibika haraka hata kabla hujavifaidi? Kama ndiyo, basi sahau kupoteza fedha yako kwani unaweza ukatumia vigandishio vya barafu kugandisha viungo vyako.
Chukua viungo vyako na vikate kufikia kiasi utakacho, weka viungo vyako kwenye vigandishio vya barafu (Ice trays) na kisha weka mafuta ya kupikia kiasi ili vigande.
Kwa kufanya hivyo, hautahitaji kutumia mafuta endapo utavitumia kwani mafuta uliyoyagandisha na viungo yatakutosheleza. Sasa unaweza kuepuka kutupa viungo vyako kwa kisingizio ya kuharibika. Hata hivyo, mbinu hii siyo rafiki kwa vitunguu swaumu.
Dondoo muhimu bado zinaendelea. Baki kwenye ukurasa huu uzidi kuzifaidi.